March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANAPA yamuonesha Jenerali Waitara Faru mwenye jina lake

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

KATIKA kuenzi mchango mkubwa wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini – TANAPA, Mkuu wa Majeshi (Mstaafu) Jenerali George Waitara kwa uanzishwaji wa zao jipya la utalii wa kuwapa majina Faru (Rhino Naming), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia Hifadhi ya Taifa Mkomazi iliyopo wilayani Same mkoa wa Kilimanjaro, imemuonesha rasmi faru aliyepewa jina lake “Faru Waitara” leo Septemba 21, 2025.

Lengo la kufanya hivyo ni kutambua mchango wake katika masuala ya Uhifadhi na Utalii yaendelee kutamalaki kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.

Kuwapa wanyamapori majina ya watu ni pamoja na kuwatangaza, kuwaweka wanyama hao karibu na jamii hivyo kupunguza kasi ya kuwaua wakihisi kuwa wanamuangamiza yule aliyetoa jina.

Vile vile huongeza hamasa ya wananchi kwenda kuwaangalia na kujua mwenendo na maendeleo ya wanyamapori hao.

Katika hafla hiyo Jenerali Waitara amelipongeza shirika kwa kusimama kidete kuzalisha na kuwalinda wanyama hao Adimu ambao kwa takribani miongo 3 kuanzia mwishoni mwa miaka 1970 hadi mwishoni mwa 1990 walikuwa hatihati kutoweka katika uso wa Dunia.

Tangu zao hilo la kuwapa Faru majina kuanzishwa hadi kufikia sasa Faru watatu (3)wameshapewa majina ambao ni Faru Azam, Alteza na Waitara.

Aidha, Mkuu wa hifadhi hiyo, ACC Emmanuel Moirana ametaja mazao mengine yanayomuhusisha Faru ni pamoja na Kumuasili Faru (Rhino Adoption), Rhino Capturing, Rhino viewing na Rhino Tracking.

Amesema, Mazao yote hayo matano (5) ni kumfanya mtalii afurahie na kupata thamani ya fedha anazowekeza katika suala la kutembelea Hifadhi za Taifa nchini.

Tukio hilo la kihistoria na muhimu katika sekta ya Uhifadhi na Utalii pia, lilihudhuriwa na Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara – TANAPA, Massana Mwishawa.

Wengine ni, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Kamanda wa Kanda ya Kaskazini Steria Ndaga, ACC Emmanuel Moirana Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi, ACC Catherine Mbena, Makamishna Waandamizi, Maafisa na Askari wa Uhifadhi – TANAPA.