January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANAPA wakamilisha zahanati Korogwe

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limefanikisha kukamilisha ujenzi wa zahanati Kijiji cha Kweisewa, Kata ya Mkalamo, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga kwa gharama ya milioni 72.0.

Kabla ya ukamilishaji huo, wananchi walianza ujenzi huo na kufikia hatua ya renta huku kazi zilizokamilishwa na TANAPA ni kupiga ripu, kuweka dari, kupaua na kuezeka, kutengeneza milango na madirisha, kuweka sakafu, kufunga mfumo wa umeme, kuweka mifumo ya maji, kupiga rangi na uwekaji wa samani.

Kamishna wa Uhifadhi TANAPA Mussa Kuji alipokuwa anatoa taarifa ya ujenzi wa zahanati ya Kweisewa mbele ya Waziri wa Maliasili na Utalii Angella Kairuki

Hayo yalisemwa na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA Mussa Kuji wakati akisoma taarifa ya ujenzi huo mbele ya Waziri wa Maliasili na Utalii Anjella Kairuki kwenye hafla ya uzinduzi wa zahanati hiyo uliofanyika Kijiji cha Kweisewa.

“Mradi huu ulianza kutekelezwa rasmi Machi 3, 2023 na kukamilika kwa wakati ambapo hadi kukamilika kiasi kilichotumika ni milioni 72.0 huku gharama ya mradi ilikua milioni 73.8ambao umetekelezwa na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kwa kushirikiana na wananchi wa Kweisewa pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe,” amesema Kuji.

Kuji amesema, mradi huo ni matunda ya faida za uhifadhi zinazotokana na kuongezeka kwa idadi ya wageni na mapato yatokanayo na utalii katika hifadhi za Taifa ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ambayo imepakana na Wilaya ya Korogwe.

Waziri wa Maliasili na Utalii Angella Kairuki akihutubia kadamnasi kwenye Kijiji cha Kweisewa

Mradi huo umetekelezwa ili kusaidia upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa Kijiji cha Kweisewa waliokuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita 30 kufuata huduma za matibabu, ushauri, tiba mbalimbali na kliniki katika vituo binafsi.

Pia mradi utasaidia kutoa hamasa kwa wananchi katika kushiriki na kuthamini shughuli za uhifadhi.

Aidha amesema mradi huo ni moja ya miradi sita iliyotekelezwa na TANAPA kupitia Hifadhi ya Taifa Mkomazi kwa mwaka wa fedha 2023/2024, ambapo zaidi ya milioni 765 zimetumika katika miradi ya jamii.

Huku Wilaya ya Korogwe imenufaika na miradi miwili iliyogharimu milioni 248 ikijumuisha ukamilishaji wa zahanati ya Kweisewa na ujenzi wa kituo cha Polisi Kalalani.

“Uboresha wa miundombinu ya utalii kupitia miradi ya UVIKO 19, kutangaza utalii ndani na nje ya nchi hasa kupitia filamu maarufu ya The Royal Tour hizi kazi nzuri za Rais ambazo zimeongeza idadi ya wageni kwa TANAPA ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ambayo wageni wameongezeka kutoka 3,334 mwaka 2019/2020 hadi kufikia wageni 7,920 mwaka 2022/2023,”amesema Kuji na kuongeza

“Kwa mwaka 2023/2024, hadi kufikia mwezi Februari, jumla ya wageni 6,371 wameshatembelea Hifadhi ya Taifa Mkomazi,”.

Waziri wa Maliasili na Utalii Angella Kairuki akipeana mikono na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Sadick Kallaghe alipowasili Kijiji cha Kweisewa kwa ajili ya uzinduzi wa zahanati ya kijiji hicho

Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini Timotheo Mnzava, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii, amewapongeza TANAPA kwa kazi nzuri kuanzia aliyekuwa Kamishna wa Uhifadhi TANAPA William Mwakilema ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, ambaye yeye ndiyo alipokea ombi la wananchi wa Kweisewa kumaliziwa zahanati hiyo.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Anjella Kairuki amewapongeza wananchi kwa kuendelea kuwa walinzi wazuri wa maliasili za Taifa ikiwa ni pamoja na kupambana na ujangili wa wanyama ikiwemo tembo kwenye maeneo yao.

“Kwani kwa kulinda hifadhi zetu na kuwalinda wanyama utalii unaongezeka na mapato yatokanayo na utalii yanaongezeka, hivyo kuifanya TANAPA kutenga fedha za kuhudumia jamii inayozunguka hifadhi hizo,”amesema Kairuki na kuongeza kuwa:

“Kuanzia Januari hadi Novemba mwaka 2023 watalii kutoka nje ya nchi walikuwa 1,800,008, hiyo ni kazi nzuri iliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii kupitia filamu yake ya Royal Tour.Hivyo fedha zilizotokana na utalii ndiyo hizi zinaletwa kwenu kwa ajili ya shughuli za jamii,”.

Ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi kujiepusha na vitendo vya ujangili pamoja huku akiwataka kutoa taarifa endapo wataona mtu anayetenda vitendo hivyo.

Waziri wa Maliasili na Utalii Angella Kairuki akipata maelezo kutoka kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Miriam Cheche ni wakati anaangalia maeneo ya kutolea huduma kwenye zahanati ya Kweisewa
Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini Timotheo Mnzava akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Zahanati ya Kweisewa