Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
SHIRIKA la hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), limesema litawachukulia hatua kali waliowaongoza watalii kushuka kwenye magali katika eneo la Kogatende kivuko namba nne, katika hifadhi ya taifa Serengeti bila ya kufuata sheria.
Julai 21, 2025, zilionekana picha jongefu na za mnato katika mitandao ya kijamii zikionyesha watalii wakiwa wameshuka kutoka kwenye magari katika eneo la Kogatende, kivuko cha wanyama aina ya Nyumbu kwenye hifadhi hiyo.
Akizungumzia hilo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi ambaye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TANAPA, Catherine Mbena amesema tayari wameyabaini magari yote yaliyohusika katika kadhia hiyo na hatua kali zimeanza kuchukuliwa dhidi ya waongoza watalii.
“Ni kweli tukio hilo limetokea leo (jana) tarehe 21/07/2025 ambapo watalii waliruhusiwa kushuka kwenye magari na madereva wanaowaongoza katika eneo la Kogatende, mto Mara hifadhi ya taifa ya serengeti, wakiwa wakiwaangalia nyumbu wakivuka katika mto huo.

“Kama ilivyo kawaida, msimu huu ni msimu wa mara crosing, na Nyumbu uvuka kutoka upande mmoja wa Serengeti kuelekea upande mwengine.
“Eneo hilo linawavuta watalii wengi kuja kuliangalia, ni eneo ambalo huruhusiwi kushuka kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu za Hifadhi za Taifa Tanzania,” amesema Kamishna Catherine Mbena.
“lfahamike kwamba Kitendo cha kushuka kwenye magari kinaharibu utaratibu mzima wa msafara wa Wanyama, Uharibifu
wa Mazingira na pia kuhatarisha usalama wa watalii kwani msafara huo wa nyumbu huambatana na Wanyama wanaokula nyama kama Simba, Chui, Fisi na wengine,” ameongeza.
Hata hivyo amesema, baada ya tukio hilo la watalii kushuka kutoka kwenye magari, askari wa TANAPA kutoka kikosi cha Kogatende walifika eneo la tukio na kuwaelekeza watalii hao warudi kwenye magari yao na kwamba kushuka katika maeneo hayo ni kinyume na utaratibu.
“Siku zote watalii uwasikiliza waongozaji, chochote wanachowaambia wao hufanya. Tungetegemea waongoza watalii hawa wangefuata utaratibu, sheria na kanuni.
“Natumia nafsi hii kuwaelekeza taratibu, sheria na kanuni za hifadhi kwanza kwa usalama wao, pili kwa usalama wa wanyama lakini tatu kwa ajili ya kutunza Ikolojia ya eneo husika,” amesema.
Aidha, amesema baada ya kuyabaini magari hayo, TANAPA itachukua hatua kali za kudhibiti vitendo hivyo na hatua hizo kali zinakuja baada ya kuwa na mlolongo wa vikao na wadau.

“Tukielekezana namna nzuri ya kufuata utaratibu ili wakati wa kuwa na utalii huu wa kuangalia wanyama aina ya nyumbu, watalii wanaotoka mbali kuja kushuhdia kivuko hicho cha wanyama waweze kuridhika na kile ambacho wanakuja kukiona.
“Hawawezi kuridhika katika mazingira ya vurugu kama yanayoonekana kwenye picha ambazo leo zimeonekana,” amesema Kamishna Mbena.
Amesema, kutokana na hilo hatua kali kali za kinidhamu zitachukuliwa. TANAPA imekuwa ikichukua hatua kali lakini kwa tukio hilo watachukua hakua kali zaidi ili kuwapa ujumbe kwamba wanachoongea kwenye vikao wanamaamisha.
“Tunaendelea kuwakumbusha wadau wote kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Hifadhi za Taifa Tanzania.
“Sisi kama TANAPA, tutaendelea kuyalinda haya maenekeo kwa weledi na umakini kwa ajili vizazi vijavyo.
“Tunaendelea kuwakaribisha wageni, watalii wa ndani na wa nje kuja kuangalia mali asili ambazo tumejaliwa na Mwenyezi Mungu,” amesema Kamishna wa Uhifadhi, Catherina Mbena.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina