Na.Mwandishi Wetu,TimesMajira
KATIKA kuendeleza juhudi za kulinda mazingira na vyanzo vya maji, TANAPA imepokea ufadhili wa Msitu wa Burka uliopo Ngaramtoni ya Chini, Arusha, wenye ukubwa wa ekari 76.3.
Kupitia ufadhili huo, TANAPA iliingia mkataba na Kampuni ya Burka Coffee Estates Limited na kwa makubaliano hayo, TANAPA itakuwa na jukumu la kuulinda na kuutunza msitu huo ili uendelee kuwa msitu wa asili na eneo muhimu la kuhifadhi vyanzo vya maji.
Uhifadhi huo utahusisha kulinda miti na mimea ya asili, wanyamapori, chemchemi na vyanzo vya maji, pamoja na kuhakikisha shughuli zinazoweza kuharibu mazingira hazifanyiki.

Wakati akikabidhi Msitu huo, Alex Rechsteiner, Mkurugenzi Kampuni ya Burka Coffee Estates Limited ameeleza kuwa wamefurahi kumpata mdau sahihi ambaye jukumu lake kubwa ni uhifadhi endelevu na hivyo, wanaamini kuwa TANAPA itaendelea kuutunza Msitu huo kwa ufanisi zaidi.
Aidha, ameeleza kuwa kama ambavyo TANAPA iliomba awali, inaweza kutumia msitu huo kwa shughuli za utalii kwa wanyamapori ambao hawaleta usumbufu kwa jamii na wanaoendana na mazingira ya Msitu huo.

Akizungumza wakati makabidhiano hayo kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara, Izumbe Mgana Msindai, amesema kuwa TANAPA imeupokea kwa furaha Msitu huo na kuthamini dhamana hiyo ya uhifadhi, ambayo ni sehemu muhimu ya juhudi za kulinda mazingira na kuhakikisha uendelevu wa vyanzo vya maji.
Amesisitiza kuwa TANAPA itatekeleza wajibu wake kwa kuhakikisha msitu huo unalindwa, unatunzwa na kuendelezwa kwa kuzingatia misingi ya uhifadhi endelevu, ili kuendelea kuwa urithi wa mazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, ametoa shukrani kwa Alex Rechsteiner, Mkurugenzi Kampuni ya Burka Coffee Estates Limited kwa makabidhiano hayo, akieleza kuwa ushirikiano kati ya Kampuni hiyo na TANAPA ni nguzo muhimu katika kufanikisha uhifadhi wa rasilimali za asili nchini.

More Stories
Wakulima Ruvuma kunufaika na mfumo wa stakabadhi za ghala
Tanzania,Zambia wajadili mikakati ya Ushirikiano Sekta ya Mafuta
Bimani aitaka SMZ kuchukua hatua kupunguza bei za Mafuta