January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tamwa:Tumefanya mijadala mbalimbali kukomesha rushwa ya ngono vyumba vya habari

Na Penina Malundo, timesmajira

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimesema ili kuhakikisha wanakomesha vitendo rushwa ya ngono ndani ya vyumba vya habari
wamekuwa wakifanya mijadala mbalimbali na waandishi wa habari ili waweza kufahamu kuwa rushwa hiyo ni kosa la jinai.

Hayo yalibainishwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Dk. Rose Reuben wakati wa semina ya siku moja iliyoandaliwa na Tamwa kwa kushirikiana na Mfuko wa Udhamini wa Wanawake Tanzania (WFT-T) kupitia mradi wa kuangazia rushwa ya ngono kwa wanahabari wanawake

Dk. Reuben amesema wemekuwa wakiwasaidia waandishi wa habari kupata uelewa zaidi ili kuwakumbusha kuwa yule mtu mwenye kutengeneza mazingira ya kufanya hayo tayari anakuwa anakinzana na sheria na kuharibu tasnia ya habari.

“Ukatili wa kingono na kijinsia katika vyombo vya habari unaathiri hata maudhui ambayo tunayatoa kwa umma na inawezekana kwamba sisi ndio sababu ya ukatili huo kuendelea kutokana na kwamba hatuwezi kuweka wazi maudhui ambayo tunafanyiwa sisi nyuma ya pazia,” amesema.

Aidha amesema Tamwa ilifanya utafiti 2022 uliothibitisha kuwapo kwa vitendo hivyo vya rushwa ya ngono na udhalilishaji mwingine katika vyombo vya habari ukiwamo wa kimwili na maneno

“Utafiti huu ulionesha kwamba zaidi ya asilimia 68 ya waandishi wa habari wanawake walikuwa wameathiriwa na vitendo hivi vya rushwa ya ngono, pia ulionesha wanawake hao hawakuwa tayari kuzungumza kwa sababu hawaoni msaada mbele yao huku wengine waliona kwamba ni aibu kuzungumza masuala hayo,”amesema na kuongeza

“Wengine hawakuwa tayari kuzungumza kwa sababu walikuwa wanalinda kazi zao hivyo wanapambana hivyo hivyo kimjini mjini ili mradi aendelee na kazi yake,” amesema Dk. Reuben.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mstaafu wa Tamwa, Dk. Ananilea Nkya amesema rushwa ya ngono inaweza kukomeshwa na waandishi wa habari wanawake wenyewe kwa kuinuka na kufanya kazi kwa bidii huku wakijiwekea malengo ya kufika mbali zaidi.

“Ni muhimu kuhakikisha unafanya kazi kwa bidii na kuacha uzembe ukiwa kazini, weka malengo yako binafsi na uweze kuyafikia, heshimu kila mtu, andika stori nyingi hadi bosi wako kazini ashangae, ukifanya hayo heshima yako itakua kazini na rushwa ya ngono itakupitia mbali,” amesema Nkya

Naye Mchunguzi Mkuu na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni, Bibie Msumi amesema nao wamefanya utafiti na kubaini uwepo wa rushwa wa ngono katika taasisi za elimu ya juu huku watu wengi waliokamatwa kwa makosa hayo ya rushwa ya ngono ni wahadhiri wa vyuo vikuu na vya kati.