Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Adolf Ndunguru amesema utoaji wa ajira kwa walimu 4,633 wa masomo ya Elimu ya Biashara na Amali haukuwa tu hatua ya kuziba pengo la upungufu wa watumishi, bali ni ushahidi wa dhamira pana ya Serikali ya kuimarisha utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa ya mwaka 2023.
Aidha, Serikali haikuishia kutoa ajira, bali ilihakikisha kuwa walimu hao wanapitia mafunzo elekezi na ya kina, ili kuwawezesha kutekeleza kwa ufanisi mahitaji mapya ya ufundishaji na ujifunzaji unaolenga umahiri.

Ameyasema hayo Juni 28, 2025 wakati anafunga mafunzo maalumu ya walimu wa ajira mpya wa masomo ya Elimu ya Biashara na Amali kwa shule za sekondari za Serikali Tanzania Bara kwenye Chuo cha Ualimu Korogwe mkoani Tanga, na walimu 1,670 walishiriki mafunzo hayo, ambapo
kituo cha Chuo cha Ualimu Morogoro 640, Chuo cha Ualimu Korogwe 442 na Chuo cha Ualimu Tabora 588. Miongozi mwa walimu waliopata mafunzo hayo, 1,056 ni walimu wa somo la Elimu ya Biashara, 239 ni walimu wa Amali, na walimu 375 ni mafundi wa maabara (Lab Technician).
Ndunguru amesema wanapofunga mafunzo hayo ya siku 10, hawawezi kusahau mchango mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia uratibu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kuweka alama ya kipekee katika historia ya elimu nchini.
“Mafunzo haya yamejikita pia katika kuimarisha uwezo wa walimu kushughulikia changamoto zinazowakabili wanafunzi katika muktadha wa kijamii ikiwemo malezi, maadili, afya ya akili, na ujenzi wa utu wa kijana wa Kitanzania. Kupitia mafunzo haya Serikali imewapa silaha muhimu siyo tu za kitaaluma, bali pia za kijamii na kimaadili, ili waweze kuwa walimu, walezi na viongozi katika shule mnazofundisha” amesema Ndunguru.

Kwenye hotuba yake iliyosomwa na Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (anaeshughulikia elimu) Atupele Mwambene, Ndunguru amesema
hatua hiyo inaonesha kwa dhahiri kuwa Serikali haitoi tu ajira kwa walimu, bali inawekeza kikamilifu katika kuwajengea uwezo ili wawe mawakala wa mabadiliko chanya shuleni na kwenye jamii kwa ujumla. Huo ni ushahidi tosha wa uongozi wa kisera unaoona mbali na unaojali maendeleo ya watu kama nyenzo ya maendeleo ya Taifa.
“Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuonesha dhamira ya kweli ya kuimarisha elimu nchini kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha walimu kujiendeleza kitaaluma wakiwa kazini. Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuwezesha walimu wapya wa ajira kujiunga na mafunzo ya Postgraduate Diploma in Education kupitia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, kwa mfumo unaowawezesha kuendelea na majukumu yao katika vituo vyao vya kazi.
“Mpango huu unalenga kuhakikisha kwamba ndani ya kipindi cha miaka mitano, kila mwalimu anakuwa amekamilisha sifa za kitaaluma zinazotakiwa kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma, huku akiendelea kuchangia kwa ufanisi katika utoaji wa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania.
Hii ni hatua muhimu inayoonesha kwamba Serikali haioni ajira ya mwalimu kama hitimisho, bali kama mwanzo wa safari ya kukuza uwezo, maarifa na weledi. Nawahimiza muitumie fursa hii kwa uzalendo na dhamira ya dhati ya kujenga taifa kupitia taaluma yenu” amesema Ndunguru.

Ndunguru alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wahitimu kuwa ualimu ni taaluma ya kipekee iliyojaa uzito wa kijamii na kiutaifa. Ni wito unaohitaji siyo tu maarifa na ujuzi, bali pia moyo wa kujitolea, nidhamu ya hali ya juu, na maadili thabiti ya kitaaluma. Katika mazingira ya sasa ya mabadiliko ya mitaala na mitazamo ya elimu, mwalimu anategemewa kuwa kiongozi wa maarifa, mlezi wa maadili, na mwezeshaji wa ujenzi wa umahiri kwa wanafunzi.
“Ni matarajio ya Serikali kwamba kila mmoja wenu atarejea shuleni akiwa amebeba ujuzi wa kisasa wa kufundisha, masomo yenu lakini pia mtakuwa walezi wa watoto maowafundisha. Endeleeni kuwa mabalozi wa mabadiliko ya kielimu kwa kutumia mbinu shirikishi, zinazozingatia mazingira ya mwanafunzi na jamii inayomzunguka. Vilevile, hakikisheni mnaendeleza jitihada za kitaaluma kwa kufanyia kazi yale yote mliyoyapata katika mafunzo haya.
“Nawasihi pia mjikite katika kuziishi kwa vitendo kanuni na taratibu za utumishi wa umma, huku mkiwa kielelezo cha maadili ya taaluma ya ualimu katika maeneo yenu ya kazi. Uadilifu, uwajibikaji, na uzalendo viwe dira yenu ya kila siku, mkilenga siyo tu kufundisha, bali kulea na kuongoza kizazi cha sasa kuwa raia bora wa kesho. Mkiwa sasa mmewezeshwa kielimu na kitaaluma, matumaini yetu ni kuwa mtakuwa walimu wa mfano, mnaochanganya umahiri wa kitaaluma na ubunifu wa kitaalamu katika kufanikisha malengo ya kitaifa ya elimu bora na jumuishi kwa wote” alisema Ndunguru.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) , Dkt Aneth Komba alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea walimu uelewa kuhusu taaluma ya Ualimu, uwezo wa kutumia mbinu stahiki za ufundishaji na ujifunzaji darasani, uandaaji wa masomo na kutoa ushauri wa kitaaluma na malezi kwa wanafunzi. Aidha, umahiri mahususi uliowezeshwa katika mafunzo hayo ni pamoja na kujenga uelewa kuhusu taaluma ya ualimu, kujenga uelewa kuhusu majukumu ya mwalimu katika utekelezaji wa mtaala na masuala mengine ya kijamii katika maisha ya wanafunzi shuleni.

“Kukuza uelewa kuhusu mtaala na mihutasari ya Elimu ya Amali na Biashara, kumudu mbinu mbalimbali za ufundishaji na ujifunzaji, kumudu mbinu za upimaji na tathmini, kumudu mbinu za kufaragua zana na namna ya kuzitumia katika ujifunzaji na ufundishaji, kumudu mbinu za kufanya maandalizi ya ufundishaji ikiwemo uandaaji wa Azimio la Kazi na Andalio la Somo, na
kufanya ufundishaji onesho kwa kutumia mbinu na zana mbalimbali” alisema Dkt. Komba.
Dkt. Komba alisema wawezeshaji wa mafunzo hayo ni wakufunzi kutoka vyuo vya ualimu nchini, ambapo katika kituo cha Chuo cha Ualimu Korogwe wapo wawezeshaji 12, Chuo cha Ualimu Tabora 15 na Chuo cha Ualimu Morogoro 15.
“Pamoja na mafunzo haya, TET, imeendelea kuandaa moduli na maudhui ya kidigitali kwa ajili ya Mafunzo Endelevu kwa Walimu Kazini. Moduli hizi zimepandishwa katika Mfumo wa Ujifunzaji (Learning Management System-LMS). Lengo ni kuhakikisha kuwa mafunzo ya walimu yanakuwa endelevu na walimu wanaendelea kujifunza zaidi kupitia mfumo huo pamoja na kushiriki Jumuiya za Kujifunza (JzK) ili waweze kuimarisha uwezo wao zaidi wa kutekeleza mtaala kwa ufanisi. Ombi letu ni kuomba walimu waendelee kushiriki MEWAKA na kutumia mfumo huu wa ufundishaji na ujifunzaji” alisema Dkt. Komba.

Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Mji Korogwe, Mary Mmary aliwaasa walimu kuwa kupata mafunzo ni jambo moja, lakini kuyafanya mafunzo hayo kuisaidia jamii ni jambo jingine, hivyo walimu hao waende kuibadilisha jamii kwenye kuleta maendeleo.
Naye Mkuu wa Chuo cha Ualimu Korogwe Hassan Ismail alisema wao kama chuo wamejipanga kuona maboresho ya kielimu yanayofanyika nchini, huku chuo hicho ikiwa ni moja ya vyuo vya kufanikisha malengo hayo, wataendelea kutoa huduma bora na mazingira mazuri yakufundishia.


More Stories
TAMWA yakumbusha jamii kupinga ukatili wa kijinsia kuelekea siku ta wanawake Duniani
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro