October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tamisemi yaanza kwa ushindi Chanedo Cup

Na Nuru Mkupa, Timesmajira Online Dodoma

TIMU ya netiboli ya Tamisemi Queens imeibuka na ushindi wa goli 33-22 dhidi ya timu ya wanaume ya Bight Boys katika m chezo wa ufunguzi wa mashindano ya Ligi ya netiboli ya Chanedo Cup.

Ligi hiyo imeanza kutimua vumbi jijini hapa kwa kuzikutanisha timu mbalimbali ikiwa ni pamoja na timu za wanaume ambazo zimekuwa kivutio kikubwa katika mashindano hayo hiyo.

Mbali na Tamisemi kuanza kwa ushindi katika mashindano hayo, lakini pia timu ya UDOM imefanikiwa kuibuka kwa ushindi wa goli 35-11 dhidi ya vijana chipukizi wa Ihumwa Drem Ream.

Pia Tamisemi Queen waliendeleza ubabe kwa ushindi kwa kuifunga timu ya Muungano Boys kwa jumla ya goli 18-16 huku pia wakiifunga bila huruma timu ya Chuo Kikuu cha Dodoma goli 40-7 pia Bright Boys ilifanikiwa kupata ushindi wa goli 32-13 dhidi ya Ihumwa Drem Team.

Katibu wa Chama cha Mchezo wa Netiboli Mkoa wa Dodoma, Caroline Kimwaga amesema, awali walitarajia Ligi hiyo kushirikisha timu nane lakini sasa yanashirikisha timu tano baada ya zingine kushindwa kuthibitisha ushiriki wake.

“Kimsingi Ligi yetu pamoja na kuwa timu zingine zimeshindwa kushiriki bado tumefanikiwa kwa viwango kikubwa kuiandaa kwani pamoja na changamoto zilizopo bado tumefanikiwa sana. Kikubwa bado tunasisitiza taasisi za Serikali na watu binafsi kuanzisha timu za netiboli ili iwe chachu ya mafanikio ya mchezo huu ndani ya Makao Makuu ya nchi,” amesema Katibu huyo.

Bingwa wa mashindano hayo atapewa zawadi ya kombe na washindi wengine watapatia vyeti vya ushiriki wao katika Ligi hiyo pamoja na zawadi zingine ambazo zitakua za mchezaji mmoja mmoja.

Kwa upande wake kocha wa timu ya Ihumwa Drem Team, John Luoga amesema, timu yake ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo imejifunza mengi na kimsingi amekipongeza chama hicho kwa kuanzisha mashindano hayo ambayo yanaonekana kuwa na mafanikio makubwa katika kupeleka mbele mchezo huo.

Lengo la michuano hiyo ni kuziandaa timu za mchezo huo kuelekea kwenye ligi mbalimbali ndani ya mkoa wa Dodoma pia kuziandaa kwenye michezo mbalimbali ya ngazi za kitaifa.