Na Penina Malundo, TimesMajira Online
TAMBO za nani mbabe zaidi zinazoendelea baina ya wakali wa mchezo wa ngumi hapa nchini, Twaha Kassim ‘Kiduku’ na Abdallah Pazi ‘Dula Mbabe’ zitaenda kumalizwa rasmi katika pambano la wawili hao litakalofanyika Julai 24, mwaka huu ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Kwa mara ya kwanza ubinsi huo ulishindwa kumalizwa Oktoba 21 mwaka 2017 katika ukumbi wa Msasani ‘Msasani Club’ baada ya pambano lililowakutanisha wawili hao kumalizika kwa sare ya pointi.
Lakini Agosti, 2020 Twaha Kiduku alimaliza ubishi huo baada ya kumchapa kwa pointi Dulla Mbabe katika pambano la kumaliza ubishi la raundi 12 uzito wa ‘Super Middle’ lililofanyika katika Uwanja wa Uhuru.
Licha ya kupoteza pambano hilo lakini bado Dulla Mbabe hakukubaliana na matokeo hayo na kuweka wazi kuwa yupo tayari kwa ajili ya pambano la marudiano na Kiduku na ikiwa atapoteza pambano hilo basi atatamka wazi kuwa bondia huyo ni mkali zaidi yake.
Kuelekea katika pambano hilo ambalo msindi ataondoka na gari mpya aina ya Toyota Crown, serikali imeahidi kutoa ushirikiano ili kufanikisha pambano hilo ambalo linasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa mchezo huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi akizungumza mwishoni mwa wiki katika Futari iliyoandaliwa na Wakala wa Michezo wa Peak Time kwa ajili ya mabondia pamoja na kumuenzi aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa nchini Tanzania (TPBO) Yassin Abdallah Ustadh aliyefariki septemba 7, 2020 aliwataka pia wadhamini kujitokeza ili kutumia fursa hiyo kujitangaza.
“Kama serikali tunalibeba jambo hili kwani hakuna kusubiri na natoa wito kwa wadhamini kujitokea kudhamini pambano hilo ambapo kwani ni fursa ya kujitangaza lakini pia kuleta maslahi kwa mabondia hao,” amesema Dkt Abbasi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Peak Time walioandaa Futari hiyo, Kapteni Selemani Semunyu amesema, tayari wameshaanza maandalizi kuelekea kwenye pambano hilo na uwepo wa Waziri Mkuu utaupa hadhi mchezo na kufungua fursa nyingi kwa wachezaji ambao wengi wao hutoka kwenye familia duni.
Hata hivyo alisema kuwa, bado wanaendelea kutafuta wadhamini ili kufanikisha pambano hilo ikiwemo zawadi ya gari ambayo wanaamini itakuwa chachu katika mchezo huo kwa matumaini yao ni kuona mchezo huo unakuwa na manufaa kwa mabondia.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania