April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Takwimu sahihi za wenye ulemavu kusaidia utungwaji wa sera

Na Penina Malundo, timesmajira , Online

Serikali imesema upatikanaji wa takwimu sahihi za msingi za Watu Wenye Ulemavu zitawezesha kutungwa kwa sera wakilishi na kusaidia kupima utekelezaji wa malengo mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Wazri Mku Sera, Bunge na Uratibu George Simbachawene kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika Kongamano la Kuwajengea Uelewa Watu Wenye Ulemavu kuhusu Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Simbachawene amesema kwa mujibu wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) yote imeweka mkazo katika kuhakikisha Watu Wenye Ulemavu sio tu wanakuwa sehemu ya mipango ya maendeleo ya nchi bali wanapewa kila fursa za kujiendeleza katika nyanja zote za maendeleo kama wananchi wengine.

“Katika kuhakikisha kuwa jamii ya Watu Wenye Ulemavu wanakuwa sehemu ya mchakato mzima wa Sensa ya Watu na Makazi, Serikali imezingatia ushiriki wao katika hatua zote za utekelezaji wa zoezi hili la kitaifa. Ushiriki wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu nchini (SHIVYAWATA) ni ishara ya ujumuishaji huo,” amesema Simbachawene.

Baadhi ya Washiriki wakifuatilia Kongamano la Kuwajengea Uelewa Watu Wenye Ulemavu kuhusu Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Ukumbi wa Jakaya Convention Centre Jijini Dodoma.

Pia ametaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania Bara, na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Tanzania Zanzibar kuendelea kuboresha mbinu za ukusanyaji wa taarifa za hali ya ulemavu nchini, kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na Watu Wenye Ulemavu kwa lengo la kuwatambua na kuwahudumia.

“Ofisi za takwimu ziendelee kujumuisha maswali yanayolenga kupata taarifa za hali ya ulemavu nchini kwenye tafiti mbalimbali zinazofanywa na Ofisi hizo na Ofisi ya Waziri Mkuu ione uwezekano wa kuanzisha mfumo wa Kiutawala wa Kukusanya Taarifa za Hali ya Ulemavu Nchini,” ameeleza

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu),Ummy Nderianaga akifafanua jambo katika Kongamano hilo.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu ,Ummy Nderiananga ameshukuru Serekali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali watu wenye ulemavu akisema kuwa wako tayari kufanya kazi kuhakikisha Taifa linakuwa na maendeleo yenye mchango wa makundi yote.

Aidha Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa ,amebainisha kwamba Ofisi ya Taifa ya Takwimu imejipanga kuhakikisha wanachukua taarifa sahihi kwa watu wenye ulemavu itakayosaidia serikali kutambua idadi na mahitaji yao

“Tumeweka maswali ya kutosha zaidi ya maswali kumi ambayo yatatusaidia kujua kwamba nani mlemavu wa aina gani,yuko wapi ,elimu yake,mahali anapoishi, ana rasirimali kiasi gani yote”amesema

Mwenyekiti shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) ,Ernest Kimaya amesema lengo la kongamano hilo ni kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu ili kuwa nauelewa na kujua umuhimu wa sensa ya watu na makazi ili wahamasike kushiriki zoezi hilo.

“Sensa ya watu na makazi kwa upande wa Watu wenye Ulemavu Tanzania Bara na Zanzibar tukishirikiana na Tume ya Takwimu tumeboresha huongozo wa uboreshaji wa Makarani wa Sensa kwenye Dodoso la Jamii,Kaya na Majengo pamoja na maelezo yaliyojitosheleza kuhusiana na Walemavu,” amebainisha.