Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Mkoa wa Mwanza,imebaini kasoro katika miradi 8 ya maendeleo yenye thamani ya sh.bilioni 6.03 kati ya 15 yenye thamani ya sh.bilioni 25.8, inayotekelezwa mkoani humu.
Pia,Mpango wa TAKUKURU Rafiki umefanikiwa na kuleta matokeo chanya katika kutatua kero zilizokuwa zinawakabili wananchi kupata huduma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza, Idrisa Kisaka,Novemba 21,2024, akitoa taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo katika kipindi cha Julai hadi Septemba, mwaka huu,amesema taasisi hiyo ilifuatilia miradi 15 ya maendeleo yenye thamani ya sh.bilioni 25.8.
“Katika ufuatiliaji huo tulibaini miradi 8 ya maendeleo ya wananchi katika sekta mbalimbali, inayogharimu sh.bilioni 6.03 ilikuwa na kasoro ndogo ndogo,tulielekeza yafanyike maboresho na tayari yamefanyika,”amesema.
Kisaka amesema utekelezaji wa Mpango wa TAKUKURU Rfiki,umekuwa na matokeo chanya,ambapo wananchi katika kata mbalimbali hupata fursa ya kuibua kero zao kupitia vikao vinavyofanyika kati yao na TAKUKURU na kuwekeana mikakati ya utatuzi.
Pia kupitia mpango huo wananchi wamewanufaika na uboreshaji wa huduma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu,nisati,barabara, maji na ardhi.
Amesema miongoni mwa manufaa hayo ni ujenzi wa shule mpya ya Kanemwa,Kata ya Kishiri, iliyowapunguzia umbali mrefu watoto waliokuwa wakifuata huduma ya masomo katika shule za Bujingwa na Bukaga,ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika zahanati ya Shadi na uongezeko la huduma katika Kata ya Luchelele wilayani Nyamagana.
Pia, wananchi wa Kata ya Mamae wilayani Misungwi walinufaika kwa kupata huduma za jamii kwa wakati baada ya kukamilishwa kwa ujenzi wa zahanati ya kata hiyo pamoja na ukarabati wa barabara ya Mwambola-Magaka.
Naibu Mkuu huyo wa TAKUKURU, amesema uchambuzi wa mfumo kuhusiana na mapato ya mauzo ya ng’ombe katika mnada wa Misasi, Misungwi,uliwezesha mapato kuongezeka kutoka wastani wa sh.milioni 2.5 hadi milioni 3, kufikia sh.milioni 7 hadi 8, sawa na asilimia 100 kwa mnada.
Amesema katika kuchambua mfumo walibaini usimamizi duni wa ukusanyaji mapato kutoka Halmashauri ya Misungwi,maofisa watendaji wasio na weledi wa kodi na biashara kutumika kukusanya mapato,ukusanyaji holela wa ushuru,uhaba wa POS na gari,wafugaji na wafanyabiashara kutofahamu umuhimu wa kulipa ushuru huo.
“Lengo la kufanya hivyo ni kudhibiti ukusanyaji wa mapato katika soko la mnada huo ili kuboresha na kuimarisha matumizi ya mifumo ya halmashauri na kuiwezesha serikali kukusanya mapato stahiki kwa ajili ya huduma na maendeleo ya wananchi,”amesema Kisaka.
Aidha,kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024,taasisi hiyo ilitoa elimu ya madhara na makatazo ya rushwa katika uchaguzi,wajibu wa wananchi kushiriki kuzuia vitendo vya rushwa kabla,wakati na baada ya uchaguzi ikiwemo kutoa taarifa za wahusika wa vitendo hivyo kwa TAKUKURU.
Kwa mujibu wa Kisaka,elimu ilitolewa kwa makundi mbalimbali ya viongozi wa dini,waandishi wa habari,Asasi za Kiraia,wafanyabiashara,wafugaji,wakulima,bodaboda, sekta binafsi na wananchi.ssss
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito