November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU yazidi kuwanasa makada wa CCM kwa rushwa

Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga

MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi ( CCM),akiwa na wajumbe 10 wa Umoja wa Wanawake wa Chama hicho,(UWT) Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga ,wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru ) mkoani Shinyanga wakituhumiwa kwa kosa la kutaka kugawa rushwa.

Kamanda wa Takukuru Mkoani Shinyanga, Hussein Mussa amesema watuhumiwa hao, walikamatwa Juni 28, mwaka huu nyumbani kwa mmoja wa viongozi wa
wakituhumiwa kwa kosa la kutaka kugawa rushwa.

Mussa amesema wajumbe hao wamekamatwa wakiwa wanajiandaa kugawana baadhi ya vitu vinavyohisiwa kutolewa na watia nia wa kutaka kugombea udiwani au ubunge.

Amewataja watuhumiwa wanaoshikiliwa kuwa ni pamoja na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Asha Makwaiya, ambaye ni mkazi wa majengo mapya Shinyanga akiwa na Katibu wa UWT tawi la Mshikamano ,Elizabeth Itete ambao waliwakusanya viongozi hao wa UWT kwa lengo la kuwagawia mashuka, vitenge na viatu aina ya Kandambili.

“Lakini pia tumewakamata wajumbe wengine 10 ambao ni viongozi wa UWT Kata ya Ngokolo ikihisiwa walikusanywa na Makwaiya ili awagawie mashuka 10, Kitenge kimoja na viatu aina ya Kandambili pea 11 ikiwa ni kishawishi cha yeye Makwaiya kuchaguliwa au kuchaguliwa kwa aliyemtuma.” Amesema

Kamanda Mussa amesema watuhumiwa hao wote wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi.

Hata hivyo Kamanda Mussa amesema majina ya wajumbe wengine 10 yamehifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kwamba hivi sasa wanaendelea kuchunguza ili kuweza kumbaini muhusika wa vitu vilivyokamatwa.

Takukuru Mkoa huo kupitia Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Shinyanga imewatia hatiani washtakiwa wawili wa kesi ya rushwa ambao wamekiri kutenda kosa la kupokea kinyume cha sheria kiasi cha shilingi 159,000 wakidai kuwachukulia walengwa wakati haikuwa kweli.

Mussa amesema watuhumiwa hao ni Mhasibu wa kamati ya fedha za TASAF, Mhela Kashinje na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha za TASAF, Jisabo Dioniz walifikishwa mahakamani na Takukuru baada ya kukamatwa wakichukua kiasi hicho cha fedha kinyume cha sheria.

“Washtakiwa wote wawili wamehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga Juni 30, mwaka huu kutumikia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja gerezani au kulipa faini ya shilingi 500,000 kila mmoja ambapo wote wamelipa faini hiyo na kuachiwa huru,” amesema Mussa