December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU yawapiga msasa,wanahabari madhara ya rushwa katika uchaguzi

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

MKUU wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza,James Ruge amesema watawatumia waandishi wa habari kuelimisha wananchi madhara ya rushwa katika uchaguzi,kwa sababu wanaaminika,wana nguvu na nafasi ya kuifikia jamii kupitia taarifa mbalimbali.

Akifungua kikao kazi cha siku moja cha kuwajengea uwezo waandishi wa habari mkoani humu,Agosti 25,2024 amesema kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa,lengo ni kukuza na kuhamasisha misingi ya utawala bora na kutokomeza rushwa nchini,kwa kuzuia na kushirikisha umma kwa njia ya elimu.

“Lengo ni kuongeza ujuzi na ufanisi katika kuelimisha jamii ubaya wa rushwa katika mapambano dhidi ya rushwa,tunapoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani mwakani,tuangalie namna gani tutazuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi,”amesema Ruge.

Amesistiza katika kuhakikisha wananchi wanashiriki vyema uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu,watavitumia vyombo vya habari na waandishi wa habari kuwaelimisha.

Kwa mujibu wa Ruge waandishi wa habari ni kalamu ya dhahabu, wanaaminika katika jamii,wana na nafasi ya kuifikia kupitia taarifa mbalimbali,hivyo TAKUKURU itaendea kuwatumia kufikisha elimu wananchi watambue ubaya na madhara ya rushwa.

Kwa upande wake Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Misungwi, Eli Makalla akiwasilisha mada ya nafasi ya vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya rushwa amesema kifungu cha 7(b)kikisomwa pamoja na kifungu cha 45 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( Sura ya 329) kinaitaka TAKUKURU ihamasishe ushiriki wa wadau katika kuondoa rushwa nchini.

“Tunapoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani,tunaamini tutasaidiana kuwaelimisha wananchi madhara ya vitendo vya rushwa katika jamii na uchaguzi,ni adui wa haki,inakwamisha maendeleo na ni miongoni mwa maadui ujinga,maradhi na umasikini,”amesema.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC),Edwin Soko, ameishauri TAKUKURU kuwalinda waandishi wanaotoa taarifa za vitendo vya rushwa katika chaguzi, kwani ipo mifano baadhi wamekuwa wakibambikwa kesi wanapofuatilia habari za rushwa.

Amesema nchi inapoelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa wandishi wa habari wasikubali kutumika kwa rushwa ndogo ndogo na kuiomba TAKUKURU iwalinde wanaoibua ama kutoa taarifa ya vitendo vya rushwa.

“Tunayo dhamana kubwa ya kushiriki vita dhidi ya rushwa tusiishie kuhoji TAKUKURU inafanya nini,tukosoe kwa kujenga tukiangalia uwezo na mzigo ilioubeba,bajeti,rasilimali watu na vitendea kazi vilivyopo kama tunataka kupata maendeleo na kujenga jamii salama isiyo na rushwa,”amesema.

Aidha taasisi hiyo mkoani imepanga kukutana na wadau mbalimbali kutoa elimu ya madhara ya rushwa katika uchaguzi ikianza na waandishi wa habari mkoni humu.