November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU yaonya watakao fuja fedha za UVIKO-19

Na Esther Macha, TimesMajira,Online, Mbeya

MKUU wa Taasisi  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mbeya, Denis Manumbu (pichani) ametoa onyo kali kwa watendaji na viongozi  watakaobainikak ufuja fedha za Ugonjwa wa Uviko 19 ambazo zimetolewa na Serikali kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo  katika sekta ya Afya, Elimu na barabara.

Manumbu amesema hayo leo wakati akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake juu ya utekelezaji wa shughuli za Taasisi hiyo kwa kipindi cha robo ya mwaka kuanzia julai hadi septemba.

Hata hivyo Manumbu amesema kuwa  tayari Serikali imeingiza fedha za Uviko 19 kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya na kuwaomba watendaji na viongozi wote wa serikali  wote watakaopewa nafasi ya kusimamia miradi kuwa waaminifu kujiepusha na vitendo vya rushwa.

“Ndugu zangu watumishi wa umma fedha za Uviko 19 zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa  kila Halmashauri imepewa fedha, tunaendelea kufuatilia na kufanya uchunguzi kwa yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria,” amesema Manumbu.

Hata hivyo Manumbu amesema kwamba kazi ya kuzuia na kupambana na rushwa itaendelea katika maeneo yote zikiwemo taasisi za umma na binafsi na kushauri namna bora ya kuiziba mianya hiyo.

“Natoa rai kwa wakurugenzi wa halmashauri zote za.mkoa wa mbeya kutoa ushirikiano wa hali ya juu wakati wa kutekeleza miradi ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya uvico 19 katika tawala za.mikoa na mamlaka za serikali za mitaa pindi utakapo hitajika”amesema Kamanda Manumbu

Aidha Manumbu amesema Taasisi hiyo imefanikiwa kukagua miradi yenye thamani ya sh. Bilioni tano  ambapo jumla ya taarifa 124 ilikaguliwa na kubainika na tuhuma za rushwa na makosa mengine.

Amebainisha kuwa  kati ya hizo taarifa 56 zilihusu rushwa na 68 hazikuhusu rushwa  baadhi ya kesi hizo uchunguzi umekamilika na nyingine unaendelea.

Katika taarifa yake Manumbu alizinyooshea kidole taasisi binafsi na Halmashauri kuwa kinara wa vitendo vya rushwa na kwamba Halmashauri ya Jiji la Mbeya katika kitengo cha manunuzi inaongoza kwa vitendo vya rushwa.

Ameongeza kuwa Takukuru imefanikiwa kuwapa elimu wananchi 23,749  kupitia semina mbalimbali zilizoandaliwa ili kutokomeza vitendo vya rushwa mkoani Mbeya.

Hivi karibuni Mkoa wa Mbeya ilipokea fedha za Uviko 19 kiasi cha sh. Bilioni 15 kwa ajili ya mapambano ya ugonjwa wa Uviko 19 ambazo umeisumbua dunia.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema fedha hizo zinagawiwa kwa Halmashauri kulingana na mahitaji ya kuboresha miundombinu ya Afya, Elimu, Barabara na Maji.

Amewaomba viongozi kusimamia fedha hizo kwa uaminifu ili zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.