March 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NARCO yaasa uwepo matamasha ya ulaji nyama

Na Edward Kondela,TimesMajira Online, Rukwa

KAMPUNI ya Ranchi za Taifa Limited (NARCO) imetoa wito kwa viongozi wa mikoa nchini kujenga utaratibu wa kufanya matamasha ya ulaji nyama ili kuhamasisha wananchi kuongeza wigo wa kula nyama ili kujenga afya zao na kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo nchini.

Muonekano wa nyama iliyotokana na ng’ombe bora kutoka Kampuni ya Ranchi za Taifa Limited (NARCO), wakati wa tamasha la Sumbawanga Nyama Choma Festival lililoandaliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Mkoani Rukwa. (Picha na NARCO).

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Meneja Masoko wa NARCO Bw. Immanuel Mnzava wakati wa tamasha la Sumbawanga Nyama Choma Festival lilioandaliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Mkoani Rukwa likienda sambamba na uanzishaji wa mnada katika Kata ya Pito, Kijiji cha Katumba Azimio.

Akizungumza juu ya tamasha hilo Bw. Mnzava amesema NARCO kama mdau mwalikwa kwenye tamasha hilo inahamasisha ulaji wa nyama na hasa nyama ya Kongwa Beef inayozalishwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa Limited (NARCO) ambayo ina ranchi 14 nchini ikiwemo Ranchi ya Kalambo iliyoko Mkoani Rukwa.

Bw. Mnzava aliongeza kuwa uhamasishaji huu unafanyika ili kuongeza ulaji wa nyama nchini kwa kuwa kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), ulaji wa nyama nchini kwa mtu mmoja bado uko chini ambapo ni wastani wa Kilogramu 15 kwa mwaka tofauti na pendekezo la dunia la ulaji wa Kilogramu 50 kwa mwaka.

“Ulaji unaopendekezwa duniani ni Kilogramu 50 kwa mwaka. Kwa hiyo kwa wastani kila mwananchi ili afikie viwango vya ulaji nyama vinavyopendekezwa duniani anadaiwa kuongeza Kilogramu 35 ili afikishe kilo 50 kwa mwaka, ili kufikia viwango hivyo, Tanzania inadaiwa wastani wa tani za nyama 2,100,000 kwa mwaka.” amesema .

“Hili ni soko kubwa la ndani ikiwa watanzania wote watakula nyama kulingana na viwango vinavyopendekezwa duniani. Hivyo, tunapofanya matamasha kama haya tunalengo la kuhamasisha wananchi kuongeza ulaji wa nyama, kwa kuwa nyama inajenga miili yetu na ni kitoweo kizuri na tunapoongeza kula nyama wazalishaji wetu wa mifugo na mazao yake nchini wanakuwa wamepata soko la mifugo yao na mazao yake ikiwemo nyama.” amefafanua.

Aidha, amesema kuwa lengo la matamasha la ulaji nyama nchini yataongeza soko la ndani la bidhaa za mifugo na mazao yake na kutoa fursa kwa wananchi kufurahia rasilimali zinazozalishwa nchini katika sekta ya mifugo.

Afisa Masoko kutoka Kampuni ya Ranchi za Taifa Limited (NARCO) Bw. Immanuel Mnzava (kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Bw. Joseph Mkirikiti (katikati) na Meneja wa Ranchi ya Kalambo Bw. Noel Makawia, wakati wa tamasha la Sumbawanga Nyama Choma Festival lililoandaliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, likiwa na lengo la kuhamasisha ulaji nyama nchini, ambapo NARCO imeshiriki kama mdau mkubwa wa nyama nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Bw. Joseph Mkirikiti akizungumza juu ya tamasha la Sumbawanga Nyama Choma Festival amesema ni moja ya vyanzo vya mapato na matamasha hayo yatafungua fursa ya utalii wa ndani nchini.

Amebainisha pia uwepo wa NARCO ni sehemu ya kuliongezea pia thamani zao la ngozi kwa kuwa ulaji wa nyama ukiongezeka utasababisha pia uwepo wa ngozi za kutosha katika matumizi ya viwandani pamoja na chakula.

Baadhi ya watu walioshiriki katika tamasha hilo wamesema wamefurahishwa na uwepo wa NARCO kwa kuwa imekuwa ikitoa mbegu bora za mifugo kwa maana ya ng’ombe, mbuzi na kondoo ambapo mifugo hiyo imekuwa ikitoa nyama yenye ubora mkubwa.

Afisa Masoko kutoka Kampuni ya Ranchi za Taifa Limited (NARCO) Bw. Immanuel Mnzava (kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Bw. Joseph Mkirikiti (aliyevaa kofia) na baadhi ya watendaji kutoka serikalini na wananchi, wakila nyama katika tamasha la Sumbawanga Nyama Choma Festival lililoandaliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, likiwa na lengo la kuhamasisha ulaji nyama nchini, ambapo NARCO imeshiriki kama mdau mkubwa wa nyama nchini.

Wamesema kutokana na uwepo wa nyama yenye ubora ya Kongwa Beef kutoka NARCO katika tamasha la Sumbawanga Nyama Choma Festival, wamefurahia uwepo wake na kwamba nyama ilikuwa ikiisha kwa haraka kutokana na ubora wake.

Tamasha la Sumbawanga litafanyika kila mwisho wa wiki sambamba na mnada katika Kata ya Pito, Kijiji cha Katumba Azimio.