November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Takukuru yaibua madudu, kuchunguza miradi ya bilioni 8

Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

MIRADI 27 yenye thamani ya bilioni 8.165 kati ya 35 ya maendeleo katika Wilaya za Nyamagana,Magu,Misungwi na Ilemela mkoani Mwanza inadaiwa kujengwa chini ya kiwango uchunguzi umebaini.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza,James Ruge amesema wakati akitoa taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Julai hadi Septemba, mwaka huu.

Amesema kuanzia Julai hadi Septemba 2023,TAKUKURU ilifuatilia na kukagua utekelezaji wa miradi 35 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya bilioni 13.932 ili kufahamu ubora na thamani ya fedha iliyotumika.

Ruge amesema baada ya ukaguzi taasisi hiyo imeanza uchunguzi katika miradi iliyokutwa na mapungufu makubwa lakini yenye mapungufu madogo ikiwemo kuchelewa kukamilika walishauri yarekebishwe thamani ya fedha ionekane.

“Katika hiyo miradi 35 ya sekta za afya,barabara,elimu na utawala iliyofuatiliwa na kukaguliwa,miradi 27 ya 8,165,465,816.24 ilikutwa na mapungufu mbalimbali baadhi imejengwa chini ya viwango,matumizi ya vifaa duni visivyokidhi ubora na vifaa vingine vilichepushwa,”amesema.

Ruge amefafanua miradi ya Jiji (Wilaya ya Nyamagana) ya thamani ya zaidi ya bilioni 2.68 ambapo kulikuwa na mapungufu katika ujenzi wa jengo la ghorofa la shule ya sekondari Mirongo,barabara za Isamilo International,Nyehunge, Mahina,Ofisi ya Kata Mabatini na shule mpya ya Kanenwa.

Aidha wilayani Magu inakotekeleza miradi ya bilioni 2.576 iliyobainika kuwa na kasoro ni ujenzi wa wodi ya kujifungulia,stoo ya dawa na wodi ya wanaume ya hospitali ya Wilaya ,jengo la wagonjwa wa nje la zahanati ya Busalanga,shule mpya za msingi Chief Hangaya na Kisesa,vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika shule za msingi Wita,Kanyama,Ilungu,Salisima na Bugomba.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa TAKUKURU miradi ya Wilaya ya Misungwi yenye thamani ya bilioni 2.143 ,ujenzi wa shule ya sekondari Mwambola yalitumika matofali ya chini ya kiwango,bei ya vifaa vya ujenzi wa shule ya msingi Mwabebeya ilikuwa tofauti na bei halisi,viti na meza za wanafunzi wa shule ya msingi Mwagiligili viko chini ya kiwango.

“Uchunguzi umeanza kwa miradi ya ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa ya shule ya msingi Nyabiti,pia unafanyika katika ujenzi wa barabara ya Fella-Ngereka-Nyashishi ambapo mitaro imeanza kubomoka na wakandarasi wa miradi hiyo wanatakiwa kufanya marekebisho,”amesema Ruge.

Pia katika kipindi cha Julai hadi Septemba taasisi imechambua mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya kodi ya zuio na kubaini baadhi ya halmashauri hazikusanyi kodi hiyo,uelewa mdogo wa wafanyabiashara na watoa huduma wakiwemo mafundi ujenzi (Local) kutokuwa na Namba ya Mlipa Kodi (TIN Number).

Ruge amesema kodi hiyo haikatwi moja kwa moja kutoka kwa wafanyabiashara hao wanapofanyiwa malipo ya kazi zao,kutokana na mifumo ya halmashauri kutosomana na mifumo ya TRA,hivyo wanatarajia kukutana na wadau husika ili kuwapa matokeo ya kazi hiyo waliyoifanya na kuweka maazimio ya namna bora ya kukusanya kodi ya zuio.

Ameeleza taasisi hiyo pia, katika eneo la elimu kwa umma imefanya semina 70,mikutano ya hadhara 41,uimarishaji wa klabu za wapinga rushwa 101 katika shule za msingi, sekondari na vyuo,habari tisa zenye ujumbe wa kuelimisha na kukemea vitendo vya rushwa ziliandikwa,vipindi vitano vya redio na maonesho 10.