Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Mbozi
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Songwe, wametakiwa kuanzisha mara moja uchunguzi katika mradi wa ujenzi wa kituo cha afya kilichopo Kata ya Nambinzo ,wilayani Mbozi kufuatia kusuasua kwa utekelezaji wake licha ya serikali kupeleka kiasi cha milioni 500.
Ombi la kuchunguzwa kwa mradi huo limetoa Oktoba 25, 2023 na Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Happiness Seneda, mara baada ya kufanya ziara ya kukagua mradi huo na kuonekana udhaifu mkubwa wa utekelezaji wake.
Seneda ameweka wazi kuwa hajaridhishwa na usimamizi wa mradi huo hali ambayo imesababisha kushindwa kukamilika kwa wakati ukilinganisha na maeneo mengine ambayo walipatiwa fedha kwa pamoja na tayari vituo vya afya vimekamilika na vinatoa huduma kwa wananchi.
” Kwanini mradi huu haukamiliki, haiwezekani lazima tutafute njia ya kututoa hapa, sasa wakati tunaendelea na ujenzi tutawaomba Takukuru waje hapa wachunguze kama kuna mchwa kapita na kutafuna fedha na kukwamisha mradi,” amesema Seneda.
Pia aliwaagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Abdalla Nandonde na Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) Dkt. Alex Mugeta, kuunda timu ya ufuatiliaji itakayo shirikiana na kamati za ujenzi kukamilisha ujenzi ili wananchi waanze kupata huduma.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mtendaji wa kijiji hicho , Hamis Skini,amesema hadi sasa kiasi cha milioni 500 kutoka Serikali Kuu ambazo ni fedha za tozo kilipokelewa, huku mchango wa nguvu za wananchi ukiwa ni milioni 13.8 ambazo ni gharama ya tofali,mawe, mchanga pamoja na kuchimba mashimo ya vyoo na kusaidia shughuli mbalimbali kwenye ujenzi.
Skini amesema kazi zilizofanyika ni ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, jengo la upasuaji pamoja na jengo la mama na mtoto.
Hadi kukamilika kwa mradi huo unategemea kutumia kiasi cha milioni 513 kutoka Serikali Kuu na nguvu za wananchi wa Kata ya Nambinzo.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi