Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Takukuru Mkoa Tanga imewataka wasimamizi wa miradi ya maendeleo kuzingatia uadilifu na uaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao na kwamba taasisi hiyo haitosita kuchukua hatua stahiki dhidi ya wale wote watakaofuja fedha zilizotolewa na serikali kwajili ya miradi ya maendeleo.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jijini Tanga ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi octoba hadi desemba 2022, Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa Tanga Victor Swella amesema kuwa wamejipanga na wanaendelea na uzuiaji wa rushwa katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Kaimu Mkuu wa Takukuru amesema kuwa watajielekeza kwenye ufuatiliaji wa miradi ya ujenzi katika wilaya zote za Mkoa Tanga ili kuhakikisha kwamba fedha zinazotolewa na serikali zinatumika kukamilisha miradi husika na kwa wakati na kwa ubora unaolingana na thamani ya fedha husika.
“Tumejipanga na tunaendelea na uuzaji rushwa katika ukuasanyaji wa mapato ya serikali na kipekee, tunaendelea kufuatilia mifumo ya ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki (POS) ili kuweka udhibiti madhubuti kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato, “alisema Kaimu huyo Mkuu wa Takukuru.
Aidha alisema katika jukumu la kuchunguza tuhuma au makosa ya rushwa pamoja na njama za kutendeka kwa makosa hayo wamepokea jumla ya taarifa 147na kati ya taarifa hizo 91 ni za vitendo vya rushwa na taarifa 56 sio za vitendo vya rushwa.
“Kati ya taatifa 147 zilizopokelewa, taarifa 86 zinaendelea na uchunguzi na taarifa 16 zimefungwa kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kuthibitisha tuhuma, taarifa 39 wateja walishauriwa namna ya mbadala wa kutatua kero zao na taarifa 6 zimehamishiwa idara zingine kwa hatua zaidi, “alisema Swella.
Sambamba na hayo mchanganuo wa taarifa hizo za malalamiko kisekta ni Tamisemi (Utawala 63, Elimu 16, Afya 4, Ardhi 13) Ujenzi 3, Mahakama 15, Sekta binafsi 13, Wakala wa serikali 2, Nida 1, Mifuko ya hifadhi ya jamii 2, Tasaf 1, Maji 1, Mashirika ya umma 2, NGO 1, na Majeshi ya ulinzi na usalama 10.
“Katika kipindi husika tumefungua kesi 2, mahakamani na kufanya jumla ya kesi zinazoendeshwa mahakamani kwa kioindi tajwa kuwa 32 ambapo kati ya kesi hizo maamuzi yametolewa kwa kesi 3 na jamuhuri imeshinda kesi 3,”alisema
Aidha Swella amebainisha kuwa Taasisi hiyo katika kipindi hicho cha miezi mitatu imefanikiwa kuokoa fedha za serikali kiasi cha shilingi milioni 17 katika ujenzi wa miundombinu ya madarasa 11 katika Wilaya ya Korogwe.
“Kwa ujumla kutokana na ufuatiliaji wa karibu uliofanywa na Takukuru miradi yote ya ujenzi wa madarasa 11 katika shule za sekondari Nyerere, Kimweri, na Semkiwa ilikamilika kwa wakati ns kwa gharama ya shilingi 220,000,000.00 kwa miradi yote iliyofuatiliwa badala ya shilingi 237,000,000.00 iwapo ufuatiliaji huo usingefanyika.
Ameongeza kuwa Ufuatiliaji huo umezuia hasara ya shilingi 17, 000,000.00 ambazo serikali ingepata sababu ya ukiukwaji wa taratibu katika manunuzi ya bidhaa za ujenzi wa miradi husika, kwasasa madarasa yote yanaendelea kutumiwa na wanafunzi wapya waliojiunga na elimu ya sekondari ya kidato cha kwanza mwaka 2023.
More Stories
Rc.Chalamila:Tunaendelea kuokoa majeruhi Kariakoo kwa ustadi mkubwa
Act Wazalendo yazindua ilani uchaguzi serikali za mitaa
Mhagama atoa somo kwa watendaji