November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU Ruvuma yafanya ufuatiliaji wa miradi 13

Na Cresensia Kapinga,TimesMajira,Online Songea

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Ruvuma (TAKUKURU) imefanikiwa kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo 13 yenye thamani ya sh. 1,525,158,541.

Kwenye miradi hiyo mapungufu machache yalibainika, ambayo yalitolewa mapendekezo ya maboresho kwa mamlaka husika .

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Taasisis ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ruvuma, Hassan Mwenda amesema tayari miradi miwili iliyokuwa imebainika kuwa na mapungufu makubwa ilishaanza kufanyiwa uchunguzi.

Kamanda Mwenda ametaja miradi hiyo iliyofuatiliwa kuwa ni ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi majimaji, ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya sekondari ya Matemanga wilayani Tunduru, ufuatiliaji wa vituo vya rasilimali za kilimo vya Kata ya Mbesa na Nakapanya Wilayani Tunduru.

Aliitaja miradi mingine kuwa ni ufuatiliaji wa fedha za ujenzi wa majengo ya usimamizi wa kilimo za kata ya Lusewa, ufuatiliaji wa fedha za mradi wa ukarabati wa sekondari ya Magazini, ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za mradi wa ukarabati wa chumba cha maabara Sasawala, ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za mradi wa ukarabati wa chumba cha maabara Luchili Sekondari wilayani Namtumbo, ujenzi wa mradi wa maji Kijiji cha mpepai .

Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Hassan Mwenda, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichana) leo ofisini kwake.

Amesema miradi mingine ni ujenzi wa vituo vya rasilimali za kilimo vya Kata ya Mkako na Maguu wilayani Mbinga,ujenzi wa vituo vya rasilimali za kilimo vya Kata ya kilosa, ujenzi wa chanzo na tenki la maji Likwilu, ujenzi wa vituo vya kilimo vya kata ya Lilambo na Madaba Songea pamoja na ufuatiliaji wa fedha za mradi wa ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Uyahudini vyote vikiwa na tahamani ya bilioni 1.5.

Aidha Kamanda Mwenda alisema kuwa katika kipindi cha miezi mitatu, TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma ilipokea taarifa 74 kutoka kwa wananchi kupitia vyanzo mbalimbali na malalamiko yote yalifanyiwa kazi.

Alisema kati ya malalamiko 74, malalamiko 52 yalihusu rushwa ambapo 22 hayakuhusu vitendo hivyo. Alisema malalamiko 52 yalihusu rushwa yameanzishiwa uchunguzi na taarifa 18 majalada yake yalifungwa kwa kukosa ushahidi, taarifa 29 uchunguzi bado unaendelea na taarifa tano uchunguzi wake umekamilika na tayari hatua za kuwasilisha ofisi ya Taifa ya Mashtaka mkoa unaandaliwa.