
Na Israel Mwaisaka,Rukwa
asisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU mkoani Rukwa, imefanikiwa kudhibiti vitendo vya rushwa katika miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.7 kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba mwaka 2025.
Akitoa taarifa kwa umma leo Februari 3,2026, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Rukwa Mzalendo Widege amesema taasisi hiyo ilifanya ufuatiliaji wa miradi saba ya maendeleo na kubaini mapungufu mbalimbali yaliyotolewa ushauri na kufanyiwa kazi.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU ilifanikiwa kumrejesha mkandarasi aliyekuwa ameacha ujenzi wa bweni na madarasa katika Shule ya Sekondari Mzindakaya.
Mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 380 ulisimama kwa miezi miwili kuanzia Oktoba hadi Novemba 2025 kutokana na mkandarasi kuwa na zabuni nyingi.
Baada ya mazungumzo yaliyohusisha pia Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, mkandarasi huyo alirejea kazini mwezi Disemba 2025 na mradi unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Katika kuboresha utekelezaji wa miradi, TAKUKURU ilitoa mapendekezo kadhaa ikiwemo matumizi ya wahandisi waliosajiliwa na Engineers Registration Board, mafundi kutumia vifaa vya kujikinga, kutangaza zabuni mapema kupitia mfumo wa NeST pamoja na kuimarisha vikao vya eneo la mradi na utunzaji wa nyaraka.
Kwa upande wa elimu kwa umma, TAKUKURU imeendesha semina 19, mikutano ya hadhara 15, maonesho matano, kuimarisha klabu 10 za wapinga rushwa na kufungua klabu moja mpya. Hatua hiyo imeongeza mwitikio wa wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa.
Katika uchambuzi wa mifumo, taasisi hiyo imefanya tathmini ya ukusanyaji mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo na usimamizi wa Jumuiya za Maji ngazi ya Jamii katika Wilaya ya Sumbawanga, ambapo mapendekezo yametolewa na ufuatiliaji unaendelea.
Aidha, jumla ya malalamiko 64 yalipokelewa katika kipindi hicho. Kati ya hayo, malalamiko 35 sawa na asilimia 55 yalihusu rushwa huku 29 sawa na asilimia 45 hayakuhusu rushwa.
Malalamiko yasiyohusu rushwa yalifungwa baada ya ushauri, wakati yale yanayohusu rushwa uchunguzi unaendelea.
Katika masuala ya mashtaka, kesi nne ziliendelea mahakamani na kesi mbili ziliamuliwa, ambapo Jamhuri ilishinda kesi moja.
Kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026, TAKUKURU Rukwa imepanga kuendelea kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo pamoja na mali za watuhumiwa ili kufidia hasara zinazotokana na vitendo vya rushwa.
Wananchi wametakiwa kuepuka rushwa na kuendelea kutoa taarifa kupitia simu ya bure 113 au namba ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa 0738150186.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria