December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma yaokoa mamilioni ya fedha kwa miezi mitatu

Na Cresensia Kapinga,Timesmajira,online Songea.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Ruvuma kwa kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka huu imeokoa sh.102,968,122 kutokana na chunguzi mbalimbali ambazo zinaendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari leo kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi za TAKUKURU zilizopo Mahenge, Manispaa ya Songea kaimu mkuu wa taasisi hiyo mkoani Ruvuma, Owen Jasson amesema fedha hizo ni zile ambazo zilikuwa zichepushwe kwa njia za udanganyifu au rushwa ili zifanyiwe ubadhirifu kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa 11 ya mwaka 2007.

Amefafanua kuwa katika Wilaya ya Songea sh. 62,082,410 ziliokolewa, ambapo kati ya fedha hizo sh. 870,000 ziliokolewa kutokana na uchunguzi unaoendelea katika Vyama vya Kuweka na kukopa (SACCOS) wilayani humo.

Amesema sh. 55,00,000 wamelipwa wakulima wa Songea, waliokuwa wamedhulumiwa fedha walizouza mahindi yao kwa mfanyabiashara mmoja wa kampuni ya NEW EZOE, sh. 850,000 zililipwa kwa mwananchi aliyekuwa akizungushwa kulipwa fedha zake baada ya kufanya kazi ya ujenzi.

Amefafanua kuwa sh. 3,000,000 ni fedha alizolipwa mwananchi aliyekuwa akizungushwa kulipwa fedha za mafao yake kutoka kwenye Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Tawi la Songea na sh. 150,000 ni fedha alizorudishiwa mwananchi wa Songea baada ya kuchukuliwa fedha zake kwa madai kwamba ni fedha za dhamana kwa ajili ya mtoto wake aliyekuwa amewekwa mahabusu kwenye kituo Kikuu cha Polisi cha Songea mjini.

Jasson amesema katika Wilaya ya Tunduru jumla ya sh. 6,287,500 ziliokolewa ambapo kati ya fedha hizo sh. 87,500 ni marejesho ya madeni katika chama cha kuweka na kukopa (SACCOS) ya walimu wilayani Tunduru, fedha hizo ziliwekwa kwenye akaunti ya chama hicho na sh. 3,000,000 ni marejesho kwa mtoto yatima, Shakira Majuto Mboka baada ya kudhurumiwa fedha za mirathi ya marehemu baba yake na msimamizi wa mirathi, Abdallah Mgwila ambaye ni baba yake mdogo.

Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURI) Mkoa wa Ruvuma, Owen Jasson

Akifafanua zaidi amesema zaidi kuwa sh. 5,800,000 ni marejesho ya fedha alizolipwa, Kanyinda Abdallaha baada ya kudhurumiwa na watu wa Taasisi za KACHINGE, MNANKA NA OBOCHA na sh.100,000 ni fedha zilizorejeshwa kutokana na uchukuzunguzi wa malipo ya safari hewa kwa baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.

Ameongeza kuwa katika Wilaya ya Nyasa jumla ya sh. 3,304,000 ziliokolewa ambapo kati ya fedha hjzo sh. 2,411,000 ni marejesho ya fedha za madeni kutoka kwa wanachama wa Nambawala AMCOS, sh. 52,000 zililipwa kwa Beno Naminga kutokaa kwenye kikundi cha Vicoba cha Kijiji cha Malini, sh. 841,000 ni fedha alizolipwa mstaafu wa sekta ya misitu, Thomas Millinga kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwa ajili ya kusafirisha mizigo kwenda nyumbani kwao baada ya kustaafu, lakini alikuwa anasumbuliwa kulipwa bila sababu za msingi.

Amesema katika Wilaya ya Mbinga Takukuru ilifanikiwa kuokoa sh. 21,110,000, ambapo kati ya fedha hizo sh. 110,000 ni marejesho ya kurugenzi Saccos ya Mbinga, sh. 21,000,000 ni fedha aliziolipwa mwalimu mstaafu, Yasinta Ndunguru ikiwa ni sehemu ya marejesho ya fedha zake kati ya sh. 105,000,000 alizodhurumiwa na mkopeshaji wa mbinga Mjini.

Amesema kuwa katika Wilaya ya Namtumbo sh. 10,184,212 ziliokolewa, ambapo kati ya fedha hizo sh. 2,140,000 ni marejesho ya fedha za posho walizolipwa baadhi ya watumishi wa idara ya afya Wilayani Namtumbo wakati hawakustaili malipo hayo na sh. 1,260,000 ni marejesho ya malipo ya asilimia 10 ya pato la halmashauri ya wilaya hiyo ambazo zilitolewa kwa vikundi mbalimbali vya wilaya hiyo na sh. 6,784,212 ni sehemu ya marejesho ya wadaiwa wa Libango Amcos ya wilaya ya Namtumbo.

Jasson amesema Takukuru Mkoa wa Ruvuma pia ilifanya kazi ya uchambuzi wa mifumo kuhusiana na utoaji wa vibali vya ujenzi kwenye wilaya zote za mkoa wa Ruvuma ambapo uchambuzi wa mfumo wa uendeshaji wa mashauri katika baraza la ardhi la nyumba la Wilaya ya Songea.