March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU Katavi yatoa mafunzo kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa

TAKUKURU Katavi yatoa mafunzo kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa.

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline,Katavi.

MKUU wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi Sipha Mwanjala, amesema vitendo vya rushwa havikubaliki na kamwe taasisi hiyo haitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa mpaka hapo vitendo hivyo vitakapokoma.

Sipha Mwanjala ametoa kauli hiyo wakati wa mafunzo yenye lengo la kujengeana uwezo katika mabambano dhidi ya rushwa na viongzoi wa makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo viongozi wa bodaboda/bajaji, Watendaji Kata,Walimu wa Klabu za kupinga rushwa na wafanyabiashara katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi.

Mkuu wa TAKUKURU huyo,ameeleza hayo leo ,Agosti 15,2025 ambapo amesema  vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi vimekuwa tishio kwa msingi wa demokrasia na kuathiri maamuzi ya wapiga kura huku ikiharibu uwazi wa mchakato wa uchaguzi na kuzaa viongozi wasio wajibika.

“Rushwa si kwamba tu inapotosha mwelekeo wa uwamuzi kwa wananchi bali pia inapunguza imani ya wananchi kwa vyombo vya uchaguzi na serikali kwa ujumla” Amesema Sipha.

Amesisitiza “ Mbaya zaidi hujenga mazingira ya uhasama,migawanyiko ya kijamii na kuvuruga amani ya taifa”

Katika kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madini utakaofanyika mwezi oktoba mwaka huu amesema  TAKUKURU imeona haja ya kukutana na makundi hayo ili kujadili namna ya kuzuia na kupambana dhidi ya rushwa.

Alifafanua jukumu la TAKUKURU ni kuimarisha utawala bora nchini na pale panapokuwa na vitendo vya rushwa lengo la kuimarisha utawala bora na ustawi wa jamii nchini haviwezi kufikiwa iwapo rushwa itatawala katika uchaguzi.

Afisa wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi Leonard Minja, amesema uchaguzi ni fursa ambayo wananchi wanapaswa kuutumia kutafakari mustakabali wa maendeleo katika eneo lao pamoja na kuainisha changamoto zote zinazoikabili huku wakiangalia mahitaji yao.

Minja ameeleza kwamba fursa ya uchanguzi inawawezesha wananchi kujua wamchangue mgombea yupi  kati ya wagombea waliojitokeza na sio kuona ni fursa ya kujipatia fedha ambazo kimsingi ni rushwa.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi Florence Chrisant, awali akifungua mafunzo hayo amesema jamii inatambua madhara ya rushwa na kwamba rushwa ameitafasiri kama vile ni tendo la mauwaji ambalo linapaswa kuzuiwa kwa nguvu zote na jamii.

Amesema elimu ya mafunzo hayo yanapaswa kuzingatiwa kwa washiriki kuwa mabalozi wa kutoa elimu ya madhara ya rushwa na kuhakikisha kwamba jamii inaungana kwa pamoja katika kudhibiti vitendo vya rushwa kwa masirahi na ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Vilevile mshiriki wa mafunzo hayo na mkazi wa Manispaa ya Mpanda Aman Mahella, amesema TAKUKURA inapaswa kutizama mikopo inayotolewa hususani wakati wa uchaguzi kwani ndani yake imeambatana na kauli za kampeni zinazoashiria vitendo vya rushwa.

“Mnafikiri kwanini vijana na wanawake wanapata mikopo karibu na uchaguzi?, lakini sisi tunaokuwa karibu na vikundi tunaona ujumbe unaoambatana na mikopo sio mzuri” Amesema Mahella huku akisisitiza mambo hayo yanapaswa kushughurikiwa na TAKUKURU.

Mwl. Doroth Kangozi wa shule ya msingi Nyerere Manispaa ya Mpanda, Akishiriki mafunzo hayo ameishukuru TAKUKURU kwa kazi nzuri ya kuendelea kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa ufanisi zaidi.

Mwl. Doroth amesema mafunzo hayo yamewajenga na kuwa mabalozi wa mapambano dhidi ya rushwa huku ikiwaongezea ari ya kuichukia rushwa.