Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imebaini Halmashauri ya Mji wa Korogwe, na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga zinapoteza mapato ya serikali kwa watendaji wake kushindwa kukata kodi ya zuio na kushindwa kutumia mashine ya EFD kwenye manunuzi yake.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga Victor Swela wakati akitoa mada kwenye semina ya siku moja iliyowahusisha watumishi zaidi ya 500 kwenye halmashauri hizo mbili wakiwemo Wakuu wa Idara, watendaji wa kata, Wakuu wa Shule za Sekondari na Wahasibu wao, Walimu Wakuu Shule za Msingi na Walimu wa Fedha, na Waganga Wafawidhi kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali.
Swela amesema pamoja na nia nzuri ya Serikali kuanzisha matumizi ya mashine ya EFD kwa wafanyabiashara lakini kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wafanyabiashara kuuza bidhaa na huduma kwa wateja wao bila kutoa risiti za EFD, ambapo inafanya upotevu wa kodi, kwani bidhaa husika ama huduma inakuwa imefanyika bila kulipiwa kodi.
Amesema pamoja na hayo, halmashauri wakati mwingine inajisahau kukata kodi ya zuio inapofanya malipo kwa wazabuni wake.
Kwa kawaida, kodi ya zuio inakatwa asilimia mbili kwa manunuzi ya bidhaa na asilimia tano kwa manunuzi ya huduma.
“Halmashauri ya Mji wa Korogwe pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ni mmoja wa wateja wakubwa wanaofanya manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali wakati wa utekekezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo afya na elimu lakini kumekuwa na manunuzi ya vifaa au huduma ambayo yanakosa risiti za EFD,”amesema na kuongeza kuwa
“Haya yamebainishwa katika taarifa ya Mkaguzi wa Ndani katika taarifa zake za ukaguzi wa mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023. Pamoja na hayo, imebainika kuwa kwa baadhi ya malipo yaliyofanyika, hakukuwa na kodi ya zuio iliyokuwa imekatwa na kuwasilishwa TRA” alisema Swela
Swela amesema kutokana na tatizo hilo, TAKUKURU Wilaya ya Korogwe imeamua kufanya uchambuzi wa mfumo wa manunuzi ya huduma na vifaa katika utoaji risiti za EFD na ulipaji wa kodi ya zuio katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 7 (b, c) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11/2007,kwa mujibu wa kifungu hiki, TAKUKURU ina jukumu la kufanya tafiti, chambuzi za mifumo na ifuatiliaji wa fedha za Serikali ili kubainisha maeneo yenye viashiria (mianya) ya rushwa na kupendekeza hatua au namna bora ya kudhibiti,”amesema Swela.
Swela alibainisha kuwa lengo la uchambuzi huo ni kuboresha na kuimarisha matumizi ya risiti ya EFD na ukataji wa kodi ya zuio kwenye manunuzi ya huduma na vifaa katika halmashauri.
“Lengo ni ubainisha wafanyabiashara wanaostahili kukatwa kodi ya zuio na kuhakikisha wanakatwa pia kama fedha zinazokatwa kodi ya zuio zinafikishwa TRA, na kubaini mianya ya rushwa katika manunuzi inayopelekea upotevu wa mapato ya Serikali,”amesema Swela.
Naye Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Daniel Ramadhan amesema katika kutekeleza miradi ya Serikali kwenye ngazi ya halmashauri, TRA imejipanga kuongeza mapato kwa kuhakikisha inaziba mianya yote ikiwemo halmashauri na wafanyabiashara wanapofanya manunuzi wanatumia mashine ya EFD, lakini pia kukata kodi ya zuio.
Ramadhan ameaema semina hiyo itawawezesha waganga, wakuu wa shule na wahasibu wao, walimu wakuu na walimu wa fedha kujua namna ya kukata kodi ya zuio na kutumia mashine ya EFD, kwani fedha hzo zilikuwa haziingii serikalini, lakini wakati mwingine watendaji hao walikuwa hawajui kodi ya zuio.
Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo amesema sasa TAKUKURU wanafanya jambo la maana kwa kuwapa mafunzo watendaji namna ya kukusanya fedha, kutunza fedha na kuziwasilisha serikalini, badala ya kusubiri watendaji hao wafanye makosa na kuwapeleka mahakamani.
Mwegelo amesema Serikali ni moja na watendaji wanatakiwa kuwa kitu kimoja kwa kufanya kazi kwa pamoja ili kuona Serikali inapata tija kwa kuweza kupeleka miradi ya maendeleo kwa wananchi na kuleta tija, huku akiwataka watendaji kufanya kazi kwa weledi na kuacha mazoea.
Hivyo TAKUKURU wamefanya jambo jema kuwajengea uwezo watendaji ili waweze kufanya kazi kwa weledi kwa ajili ya kukusanya mapato kupitia kodi ya zuio na mashine ya EFD, lakini pia namna ya kusimamia miradi hivyo ameomba jambo hili likafanyike kwenye maeneo mengine ya taasisi za Serikali ili kuongeza ufanisi serikalini.
“Imani huzaa imani, hivyo tukafanye kazi kwa weledi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea,tuwaeleze wanaopewa kazi za Serikali huko, kodi ya zuio ni lazima hiyo itaongezea Serikali mapato sababu miradi inayoletwa huko vijijini na kwenye kata ni mingi,kikubwa, watendaji mnatakiwa mpeleke fedha serikalini, badala ya kukaa na fedha mbichi,”amesema Mwegelo.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi