December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tahadhari yatolewa kuhusu El Nino

Na Penina Malundo, timesmajira

MMAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa juu ya mwenendo wa uwepo hali ya El Niño katika bahari ya Pasifiki na athari zake nchini huku wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazotolewa na Mamlaka hiyo.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam na Mamlaka hiyo imesema El Niño ni mfumo wa hali ya hewa unaosababishwa na uwepo wa ongezeko la joto la bahari la juu ya wastani katika eneo la kati la kitropiki la bahari ya Pasifiki.

Imesema hali hiyo huambatana na athari mbalimbali ikiwemo ongezeko la mvua, joto na hali ya ukame katika maeneo mbalimbali ya dunia ambapo ukubwa wa athari unategemea nguvu pamoja na muda ambao hali ya El Niño itadumu, na kumtegemea hali na mwelekeo wa mifumo mingine ya hali ya hewa ikiwemo mwelekeo wa upepo na joto la bahari katika Bahari ya Hindi.

“Kwa Tanzania, hali ya hii ya El Niño huambatana na vipindi vya mvua kubwa na za juu ya wastani hivyo mamlaka imeendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa ikiwemo El Niño na mifumo hiyo inaonesha kuanza kujitokeza kwa El Niño, hali ambayo inatarajiwa kuimarika zaidi kuelekea mwishoni mwa mwaka 2023.,”imesema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza

“Uchambuzi wa awali wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa El Niño itakuwa na nguvu ya wastani huku athari za moja kwa moja hazijaanza kujitokeza katika maeneo ya nchi yetu kwa kipindi hiki cha Kipupwe.,”Imesisitiza.

Aidha, Mamlaka imesema inaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo mbalimbali ya hali ya hewa kwa ukaribu na kufanya uchambuzi wa kina utakaoainisha athari za El Niño katika mifumo ya mvua hususan msimu wa mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba), 2023 na taarifa hiyo itajumuisha ushauri stahiki kwa sekta mbalimbali na itatolewa kabla ya kuanza kwa msimu.

Imesema kwa msimu wa Kipupwe (Juni-Agosti), 2023 ambao bado unaendelea kama taarifa ya utabiri ilivyotolewa mwezi Mei, 2023. Vipindi vya upepo mkali pamoja na baridi vimeendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali ya nchi.” Hali ya baridi kali imeendelea kujitokeza katika maeneo ya nyanda za juu kusini magharibi (ikijumuisha mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa) na maeneo ya miinuko ya nyanda za juu kaskazini mashariki,” Imesisitiza.