October 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TADB yatoa tuzo kwa wanafunzi 13 SUA

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeshiriki katika hafla ya utoaji wa tuzo kwa wanafunzi wa SUA waliofanya vizuri katika masomo kwa mwaka 2026.
Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 7 Oktoba, 2026 ambapo TADB imeweza kutoa tuzo kwa wanafunzi 13 ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuunga mkono wanafunzi waliofanya vizuri katika taaluma zinazohusiana na sekta ya kilimo.

Akizungumza kwa Niaba ya TADB katika hafla hiyo, Bi Edna Nyatta ambaye ni Afisa Rasilimaliwatu Mkuu wa benki hiyo amesema, TADB na SUA wana makubaliano ya ushirikiano (MoU) ambapo pamoja na mambo mengine, inaiwezesha benki kutambua na kuunga mkono wanafunzi wanaofanya vizuri katika taaluma zinazohusiana na sekta ya kilimo.

Edna Nyatta amewapongeza wanafunzi hao na kuwataka kuendelea kujifunza, kuwa wabunifu na kutumia maarifa waliyoyapata chuoni kutatua changamoto zinazolikabili Taifa hususan katika Sekta ya Kilimo.

Edna ameongeza kuwa benki ilianzisha mpango wa ‘Learn with us’ ambao unatoa fursa kwa vijana kupata nafasi ya kujifunza kwa vitendo kupitia programu ya mafunzo kwa vitendo (Internship).

Amesema tayari takriban wanafunzi 10 kutoka SUA wamepata nafasi za internship kupitia mpango huo huku sita (6) kati ya hao wakifanikiwa kupata ajira za kudumu, ikiwa pia ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni kuhusiana na utekelezaji wa internship program.

TADB pia imetoa pongezi kwa SUA kwa kwa kuendelea kuzalisha wataalamu wanaohitajika katika sekta ya kilimo na kuahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano na Chuo hicho katika kukuza vipaji na fursa kwa vijana.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA, Prof. Raphael Chibunda, ameishukuru TADB kwa ushiriki wake katika utoaji wa tuzo kwa wanafunzi hao na kuiomba TADB kutoa nafasi za internship kwa wanafunzi hao 13 waliofanya vizuri na kutunikiwa tuzo katika halfa hiyo.

Amesema hatua hiyo itawasaidia wanafunzi hao kuunganisha elimu waliyoipata na uzoefu wa vitendo katika mazingira ya kazi, hatua inayoweza kuwaandaa zaidi kwa ajira na ujasiriamali katika sekta ya kilimo.