.
Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Tanga
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetumia maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Kifedha Kitaifa kutoa elimu ya kifedha kwa wananchi na wanafunzi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga jamii yenye uelewa mzuri wa masuala ya fedha na maendeleo ya kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Banda la TADB kwenye maadhimisho ya wiki ya Huduma za Fedha yanavyoendelea mkoani Tanga katika viwanja vya Usagara , Afisa Maendeleo ya Biashara wa TADB Kanda ya Kaskazini, Irene Kasegezya, amesema benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kutoa elimu ya kifedha kwa makundi mbalimbali tangu kuanza kwa maonyesho hayo Januari 19, 2026.
Alisema hadi sasa TADB imeshahudumia wananchi wengi wakiwemo wanafunzi zaidi ya 200, ambao wamepatiwa elimu ya fedha itakayowajengea msingi mzuri wa kifedha kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye.
“Tunatoa elimu ya kifedha kwa wanafunzi ili kuwajengea msingi imara wa kifedha kuanzia ngazi ya chini na kuwasaidia kuwa na desturi nzuri zitakazochangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” amesema Kasegezya.
Alieleza kuwa mbali na wanafunzi, wananchi waliotembelea banda la TADB wamepata fursa ya kushiriki madarasa ya elimu ya kifedha, ikiwemo namna ya kupanga matumizi, kuweka kumbukumbu za fedha pamoja na kujiandaa kupata mikopo.
Kasegezya amebainisha kuwa elimu ya kifedha ni nyenzo muhimu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, kwani huwasaidia kuandaa taarifa sahihi za kifedha zitakazowawezesha kupanga vizuri shughuli zao na kuhimili changamoto za kiuchumi.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Kifedha Kitaifa yanafanyika mkoani Tanga kwa kaulimbiu isemayo “Elimu ya Kifedha ni Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii.”
Afisa huyo amewahimiza wananchi kuendelea kutembelea banda la Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili kupata elimu ya kifedha, ushauri wa kitaalamu pamoja na taarifa mbalimbali zinazohusu huduma za benki hiyo.
Xxxx

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama