November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TADB yaingia makubaliano ya kimkakati na CDI, kutoa bilioni 1.15/ kwa AMCOs

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, DarIringa

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeingia katika ushirikiano wa kimkakati na Clinton Development Initiative (CDI), iliyo chini ya shirika la Clinton Foundation, ili kuweza kutoa mikopo hadi dola 500,000, sawa sawa na sh. bilioni 1.15 kwa ajili ya kufungua mnyororo wa thamani wa zao la soya mkoani Iringa.

Kulingana na randama ya maelewano iliyosainiwa hivi karibuni na mashirika hayo mawili, ushirikiano huo unalenga kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa Vyama vya Msingi ‘AMCOs’ 29 na kuwanufaisha wakulima 2,900 walio katika programu maalumu ya CDI ili kuweza kuongeza ufanisi katika uzalishaji na upatikanaji wa masoko kwa zao hilo katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa.

“TADB inayo furaha kubwa sana kuingia katika ushirikiano huu, kwa sababu ni mara yetu ya kwanza kama benki kujihusisha na mradi katika mnyororo wa thamani wa zao la soya.

Pia duniani na hapa nchini kuna ongezeko mkubwa sana la uhitaji wa zao la soya kama nyongeza ya virutubisho katika chakula cha binadamu. Kuna wakulima na wajasiriamali wadogo na wa kati, hasa wanawake, ambao wanajishughulisha na biashara hii.

Pamoja na hayo, kuna uhitaji mkubwa pia wa soya kama kirutubisho katika chakula cha mifugo pia, hususan kuku,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Japhet Justine.

Ameongeza kuwa; “Ushirikiano huu unawezesha kuwa na mfuko maalum wa mtaji kwa ajili ya kusaidia viongozi wa wakulima, mabenki ya kijamii katika vijiji ‘VICOBA’ na wanachama wa AMCOs ili waweze kupata mbegu kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora zaidi ‘Quality Declared Seeds’ (QDS) na mbegu zilizothibitishwa kuzalisha nafaka za soya.

AMCOs hizi pia zitapata mikopo maalum kwa ajili ya kuwawezesha kununua mapema mazao ya soya na kuwaunganisha katika soko la soya baada ya mavuno.”

Soya

Justine, amesema, “Uzalishaji wa soya nchini Tanzania umeongezeka maradufu ndani ya miaka 10 iliyopita. Kutoka kuzalisha tani 3,100 mwaka 2009 hadi tani 22,953 mwaka 2019. Hata hivyo, uzalishaji huu bado ni cha kiwango kidogo ukilinganisha na nchi zingine duniani.

Kupitia modeli yetu jumuishi wa kifedha wa mnyonyoro wa thamani, tuna kila sababu ya kutarajia ongezeko la uzalishaji Iringa. Tunataka kuongeza ufanisi wa uzalishaji ili kuweza kuongeza ufanisi katika kusafirisha na kuuza nje.”

Naye Mkurugenzi Mkazi wa CDI, Monsiapile Kajimbwa, alisema, “Chini ya ushirikiano huu, CDI imechangia rasilimali kwa ajili ya kufanya mafunzo ya kifedha na maendeleo ya kibiashara ya kilimo, ambapo TADB itakopesha Dola 500,000 sawa sawa na sh. Bilioni 1.15 katika hatua tofauti wa muda wa ushirikiano huu.”

Kajimbwa ameongeza kusema; “Uwekezaji huu utawaongezea kipato wazalishaji wadogo wa soya kwa sababu AMCOs zinazoshirikiana na CDI zina nafasi nzuri zaidi kuwahudumia wanachama wao.

Kwa miaka mingi, tumefanikiwa katika maeneo ya kutoa mikopo ya pembejeo za kilimo na mikopo ya shughuli baada ya mavuno kupitia vyama vya msingi tunazoshirikiana nazo. Hivyo, huu ni muda muafaka wa kupanua ukubwa wa mradi huu hapa mkoani Iringa.”

Kwa upande wake, Meneja wa Umoja wa Ushirika wa Wakulima Iringa (IFCU), Tumaini Lupola, alisema, “Hatua hii ni fursa kubwa kwa IFCU katika kuwasaidia vyama vya msingi kurasimisha uuzaji wa mazao katika masoko, hususani zao la soya kwa ajili ya kuwanufaisha wanachama na wakulima wao.

Mikopo hii itawanufaisha sana AMCOs katika kufanya ununuzi wa mapema wa zao la soya kutoka kwa wakulima wao, kukusanya na kuwauzia wanunuzi kwa idadi kubwa na viwango bora zaidi kwa namna bora zaidi.” IFCU ni wanufaika wa moja kwa moja wa mkopo huu, lakini pia watakuwa ni wasimamizi wa AMCOs hizo katika mradi huu.

Akizungumzia ushirikiano huo, kiongozi wa wakulima kutoka kijiji cha Mgama, wilaya ya Kilolo, Angelique Kitime, amesema kwamba ushirikiano huu umekuja kuokoa wakulima.

“Kuwa na uwezo wa kupata mbegu bora zilizothibitishwa na kwa gharama nafuu, itatuwezesha sisi wakulima kushusha gharama zetu za uzalishaji na kuongeza kipato chetu,” amesema Kitime.

“Baada ya miaka mitatu wa mradi huu, TADB na CDI inatarajia kuona wanachama wa AMCOs kuongeza uwezo wa uzalishaji wa soya, kuimarisha mnyororo wa thamani katika soya ambao unasimamiwa vizuri na jamii ya wakulima, na kuongeza uwezo wa kununua mapema nafaka ya soya kutoka kwa wanachama wao, pamoja na kuongeza ujuzi na maarifa yao wanapojihusisha kuuza soya katika soko la nje,” alisisitiza Mkurugenzi Mkazi wa CDI Kajimbwa.

“Mradi huu katika soya ni muendelezo wa mchango wetu muhimu katika sekta ya kilimo hapa Iringa. Mpaka Julai mwaka huu, TADB imetoa jumla ya Shilingi 5.68 Bilioni, Shilingi 2.74 Bilioni moja kwa moja, na Shilingi 2.94 Bilioni mkoani humo kupitia Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo (SCGS) kwa ushirikiano na mabenki ya kibiashara ili kuwezesha uwekezaji na muendelezo wa minyororo ya thamani kama chai, mpunga, mahindi, parachichi, maziwa, kilimo cha mboga mboga na maua, ufugaji wa kuku na pembejeo,” amesema Justine.

Katika msimu 2019-2021, CDI ilifanikiwa kuwezesha mikopo kwa wanachama 56 wa VICOBA, mikopo ya shughuli baada ya mavuno kwa AMCOs 3 mkoani Iringa, pamoja na kuwasaidia viongozi wa wakulima 106 kuthihirishwa na kuzalisha mbegu bora (QDS) kwa ajili ya wakulima wengine katika jamii zao.

CDI inafanya kazi na wakulima wadogo wapatao 80,000 nchini Tanzania, Malawi na Rwanda. Shughuli za CDI zimeweshwa kwa msaada wa shirika la Nationale Postcode Loterij.