Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Mbeya
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendelea kuvutia uwekezaji katika sekta ya maziwa sambamba na kuwahimiza wadau kuchangamkia zaidi fursa katika eneo hilo kwani lina nafasi kubwa ya kubadilisha maisha yao na kuchangia katika pato la taifa.
Akizungumza katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa mashuleni yaliyofanyika Jijini Mbeya juzi, Meneja wa Kanda wa Nyanda za juu kusini, Alphonce Mokoki ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Frank Nyabundege amesema TADB inaendelea jitihada za kuhakikisha inatoa mikopo ili kukuza uwekezaji kwenye sekta ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.
“Sisi kama benki tumejipanga na tupo tayari kutoa mikopo ili kuboresha na kukuza uzalishaji wa maziwa nchi, hivyo ni wakulima na wafugaji kuleta maombi ya mikopo ili waweze kupatiwa fedha zitakazokwenda kukuza sekta hii,” amesema Mokoki
Ameeleza kuwa TADB imekwisha toa kwa wakulima na wafugaji zaidi ya sh. bilioni 12 katika kukuza na kuendeleza mnyororo wa thamani wa maziwa kupitia vyama vyao vya ushirika hii ni kutokana na umuhimu wa sekta hiyo katika kuboresha uchumi.
“Zaidi ya wafugaji 122 kati yao wanaume 86 na wanawake 36 wamenufaika na mikopo kutoka TADB kupitia vyama vyao, aidha tunakwenda kutoa mkopo wa ng’ombe 86 kwa chama cha ushirika Wilayani Busokelo, hii ni katika jitihada za kuinua sekta ya maziwa nchini,” amesema Mokoki.
Amesema Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania ina hali ya hewa nzuri inayofaa kwa ajili ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, hivyo ni fursa kwa wafugaji wa mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe, Ruvuma na Rukwa kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kuwekezaji kwenye sekta ya maziwa.
“Sekta ya maziwa ina mchango mkubwa katika kutoa ajira kwa wananchi, kwani mbali ya maziwa kutumika kuboresha afya kwa kunywa lakini pia ni fursa ya ajira katika mnyororo mzima wa thamani wa tasnia hiyo,”amesema
Aidha, Mokoki amesema uhamasishaji wa unywaji maziwa mashuleni na katika familia ni lazima uendane sambamba na upatikanaji wa bidhaa yenyewe, hivyo TADB ipo katika kuhakikisha uzalishaji wa maziwa unaongezeka nchini na uhamasishaji unaendelea kufanyika ili kiwango cha unywaji maziwa kilichoweka kiweze kufikiwa kwa mwaka.
Kwa Upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Stephen Michael amesema Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo ambapo sensa ya mifugo mwaka 2020/2021 inaonesha Tanzania ina jumla ya ng’ombe milioni 33.9.
“Tutumie fursa hii kuongeza uzalishaji wa maziwa ambayo yataweza kulisha viwanda vilivyopo vya kuchakata maziwa nchini, na kuongeza hamasa kwa wananchi juu ya unywaji wa maziwa,” alisema Michael
Akizungumza wakati akizindua kampeni ya unywaji maziwa mashuleni yenye kauli mbiu “Faulu Mitihani kwa kunywa glasi moja ya maziwa kila siku” Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. Juma Homera amesema kampeni hii itasaidia kuondoa tatizo la udumavu nchini.
“Hii itasaidia wananfunzi kupenda masomo na kuongeza viwango vya ufaulu mashuleni, kadharika na kupunguza tatizo la udumavu nchini,” alisema Homera.
Aidha, Homera amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani hapa kutenga bajeti ya maziwa kwa wanafunzi wote wa shule za awali na msingi.
Amesema kuwa suala la unywaji maziwa shuleni kwa wanafunzi ni la lazima na si hiari.
“Hatuwezi kusubiri wadau tu kila siku wajitoa wakati watoto ni wetu wenyewe hivyo ni lazima wakati wa kupanga bajeti zote za halmashauri zilizopo mkoani Mbeya iwekwe bajeti ya kutekeleza mpango huu na kwa sababu mimi ndo naidhinisha bajeti zote,sitopitisha bajeti yoyote ambayo haina bajeti ya kutekeleza mpango huo,”amesema Homera.
Aidha Homera amepongeza juhudi na kazi inayofanywa na Wizara ya mifugo na Uvuvi kupitia bodi ya maziwa kwa kuwa karibu na wadau mbalimbali wa tasnia ya maziwa waliopo mkoani humo ambapo amewataka wasindikaji wote wa maziwa nchini kuendelea kuwekeza katika mkoa huo.
“Mimi ninapenda sana wawekezaji na kipekee kabisa niwashukuru ASAS kwa kuamua kuja kujenga kiwanda kikubwa cha maziwa hapa, niwaombe Tanga Fresh na makampuni mengine ya maziwa kufanya hivyo pia ili kuchochea zaidi uwekezaji katika tasnia ya maziwa katika mkoa wa Mbeya” Amesisitiza Homera.
Homera, ameipongeza benki ya TADB kwa jitihada zake katika kutoa mikopo kwa wakulima na wafugaji ili kuinua hali ya uzalishaji maziwa na kuchochea uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda vya kusindika maziwa nchini.
Akielezea kuhusu utekelezaji wa mpango wa unywaji maziwa shuleni, Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini (TDB) Dkt. George Msalya amesema kuwa mpango huo ulianzia mkoani Kilimanjaro mwaka 2007 kwa lengo la kuhamasisha unywaji wa maziwa nchini kwa kujenga utamaduni huo kuanzia ngazi ya shule ya awali.
“Tunafanya hivi kwa sababu mbali na maziwa kuwa lishe nzuri na kiburudisho kwa watoto, imethibitika kuwa maziwa ni mlo kamili unaoweza kujitosheleza bila kutegemea chakula kingine na ndo chakula pekee chenye virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini” Alisema Dkt. Msalya.
Aidha Dkt. Msalya amebainisha kuwa tangu kuanza kwa mpango huo takribani watoto elfu 90 kutoka shule 210 hapa nchini wamepatiwa maziwa, ambapo alisema idadi hiyo imeendelea kupungua kadri miaka inavyoendelea.
“ Tunaendelea kufanya jitihada kubwa katika kuwajengea uwezo wanafunzi, wazazi na walezi wao juu ya umuhimu wa maziwa ili kuhakikisha kiwango cha matumizi ya bidhaa hiyo kinaongezeka,” alisema Dkt. Msalya.
Maadhimisho ya Siku ya unywaji Maziwa mwaka huu yalitanguliwa na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na ugawaji maziwa katika vituo vya afya, mahabusu ya watoto na kwenye vituo vya watoto yatima.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapato