November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TADB na mapinduzi makubwa kwa wakulima, wafugaji, wavuvi nchini

Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online

UNAPOZUNGUMZIA Kilimo kina maana pana inayojumuisha mifumo ya uzalishaji mimea, ufugaji wa wanyama, na uvuvi.

Mara nyingi kilimo cha mimea kinaenda sambamba na ufugaji wa wanyama. Watu hupanda mimea na kuitunza hadi mavuno hasa kwa uzalishaji wa chakula cha binadamu na lishe ya wanyama, lakini pia kwa shabaha ya kupata malighafi mbalimbali zinazotumiwa kwa kutengeneza nguo za watu.

Siku hizi kilimo kinalenga pia nishati ya mimea. Mtu anayejihusisha na kilimo huitwa mkulima.

Kilimo ni mojawapo ya shughuli za mwanadamu ambayo humsaidia kupata mazao kwa ajili ya chakula na mazao mengine ya biashara ambayo inaweza kumuingizia kipato kwa ajili ya maisha yake, pia kipato hicho husaidia katika kukuza uchumi wa nchi ili hatimaye itakuwa imejikomboa kiuchumi.

Kwa jumla serikali zinatakiwa zitoe kipaumbele kwa sekta ya kilimo ili kuepukana na janga la njaa: mojawapo ya mahitaji makuu ya mwanadamu ni chakula.

Serikali zinatakiwa zizidi kuongeza zana za kilimo ili watu waweze kupata kwa wingi mazao ya biashara na mazao ya chakula.

Pia, serikali itoe elimu juu ya kilimo bora kama kitega uchumi ambacho huwasaidia watu kujipatia mazao na kipato cha kwao ili kuendesha maisha yao binafsi.

Wakulima wanatakiwa kupewa mikopo ya pesa, na pia kujishughulisha na kilimo cha umwagiliaji, si tu kutegemea mvua.

Nchini Tanzania, Sekta ya Kilimo ni muhimili wa maendeleo ya uchumi. Sekta hii inachangia kiasi cha nusu ya pato la Taifa, robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi na chanzo cha chakula pamoja na utoaji wa fursa za ajira zaidi ya 75% ya Watanzania.

Kilimo kina uhusiano na sekta zisizo kuwa za kilimo kupitia uhusiano wa usafishaji kwenda kwenye usindikaji wa mazao ya kilimo, matumizi na uuzaji nchi za nje, inatoa malighafi kwa viwanda na soko kwa bidhaa zilizotengenezwa.

Tanzania inazalisha takribani 97% ya mahitaji yake ya chakula. Uzalishaji wa mazao ya chakula unatofautiana mwaka hadi mwaka kutegemea kiasi cha mvua kilichopatikana.

Sekta ya kilimo inaendelea kukua na kuongeza ajira kwa vijana na wanawake, kwa kutambua hilo benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB), kupitia mfuko wake wa dhamana wa wakulima wadogo (SCGS) imetoa rai kwa mabenki nchini kujitokeza kushirikiana nao ili kuboresha mikopo kwa wakulima wadogo.

Moja ya dhamira aliyonayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt, Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha Tanzania inakuwa na chakula cha kutosha barani Afrika.

Rais Samia anasema Serikali imeshaanza kuwekeza kibajeti na kimkakati katika maeneo ya msingi kwenye kilimo, hivyo anataka Watanzania watumie vyema fursa zilizopo kuionesha dunia kuhusu sekta ya kilimo.

Pamoja na kuwekeza kibajeti na kimkakati, Rais Samia ameunda Baraza la kumshauri kuhusiana na masuala ya kilimo linaloongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Mizengo Pinda.

Ili kufikia dhamira hiyo ya Rais Samia, Wizara ya Kilimo kupitia Benki ya Mandeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kimkakati za kuwawezesha wakulima, Wafugaji pamoja na wavuvi hapa nchini.

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), ni taasisi ya kifedha ya maendeleo inayomilikiwa na serikali (DFI), iliyoanzishwa kama benki ya kitaifa ya maendeleo.

TADB, ilianzishwa chini ya Sheria ya Kampuni, 2002 CAP 212 mnamo Septemba 2012.

Lengo la kuanzisha benki hiyo ni kuongoza mikakati ya kujenga uwezo na mipango ya kuimarisha mnyororo wa thamani ya kilimo na kuunga mkono Serikali ya Tanzania miradi ya kuunda na kutekeleza sera na mikopo ya kilimo vijijini.

Benki hiyo mwaka jana ilizindua Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2023-2027), pamoja na bidhaa mpya tatu za kifedha zinazolenga kuboresha kilimo hapa nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha (Usimamizi wa Uchumi) Elijah Mwandumbya aliyemwakilisha Waziri wa fedha amesema, Serikali inafahamu umuhimu wa Kilimo kwa uchumi wa nchi na kuutambua mchango wa TADB katika kutoa mikopo yenye riba nafuu kwenye kilimo na kuongeza kuwa Serikali itaendeleo kuwekeza kwenye kilimo.

“Mwaka 2022/23, Serikali imewekeza jumla ya TZS 751.1 billioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 155.3% kutoka TZS 294.16 billioni ilizowekeza katika sekta ya kilimo mwaka uliopita.

“Ongezeko hili kubwa linadhihirisha wazi nia ya serikali kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya Kilimo,” amesema.

Naibu Katibu Mkuu ameupongeza uongozi wa TADB, pamoja na wafanyakazi kwa kukuza ufanisi wa benki hiyo kwa kuongeza wigo wa huduma zake, huku akiwahakikishia kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege amefafanua kuwa Mpango Mkakati wa TADB wa Miaka Mitano 2023 – 2027 unalenga maeneo makuu matatu.

“Eneo la kwanza ni kuleta chachu ya ongezeko la huduma za kifedha zinazotolewa na benki nyingine kwenda sekta ya kilimo, huku TADB ikiongoza katika utoaji wa huduma hizo,” amesema.

“Eneo la pili, TADB itachangia ukuaji wa mnyororo wa ongezeko la thamani kwa kutumia fursa zilizopo ndani sekta ya kilimo ili kufanikisha uwekezaji zaidi katika miondombinu ya uzalishaji, mashine, uhifadhi wa mazao, uchakataji, huduma za kimkakati na biashara ya bidhaa,

“Katika eneo la tatu, benki hiyo itazingatia kilimo cha kisasa kinachoendana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuandaa mikakati inayoshugulikia mabadiliko hayo na kuongeza uwezo wa wakulima kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi.

“Kwenye eneo la nne, tutaongeza ujumuifu kwenye hudumma za kifedha.TADB itaongeza idadi ya wanawake na vijana wanaojishugulisha na kilimo, ambapo kwa sasa wanawake ni asilimia 46% na vijana ni 44%.

“Mwisho, katika eleo la tano, benki inajidhatiti kukuza uwezo wake kwa kujenga mahusiano chanya, kukuza rasilimali fedha kwa ajili ya kilimo, kupanua wigo wa huduma zake, kujenga uwezo wa uongozi, uadilifu, kupunguza athari na kuwekeza kwa watu na mifumo bora,” amesema.

Mkurugenzi huyo amesema, TADB inaongozwa na mkakati wa muda mrefu wa miaka 20 wa kibiashara (2015-2035) ambao unatekelezwa kupitia mikakati ya kati ya miaka mitano mitano.

Katika kuhakikisha wakulima, wafugaji na wavuvi wanapiga hatua Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kupitia mfuko wake wa dhamana wa wakulima wadogo (SCGS), imefikia makubaliano ya kuongeza mkataba wa ushirikiano na Benki YA Biashara Tanzania (TCB), kwa ajili ya kutoa dhamana ya mikopo.

Nyabundege, anasema mkataba ulioingiwa kati ya pande hizo mbili ni wa awamu ya pili utaiwezesha benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kuchagiza upatikanaji wa mitaji kwa wakulima kupitia benki ya Benki ya Biashara Tanzania (TCB).

“Mikopo itakayotolewa na TCB kwa wakulima watatoa kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, mifugo na uvuvi na sisi TADB tutatoa dhamana ya hadi asilimia 70 kwa mikopo yote hasa kwa vijana, wanawake na miradi inayosaidia kupunguza au kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi,”anasema Nyabundege.

Anaongeza kwa kusema, mkataba huo utasaidia kuongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo kwa wakulima wadogo na itakua njia rahisi ya kuwafikia wengi zaidi hasa waliopo pembezoni mwa miji, mikoa na Wilaya.

hata hivyo anasema, mkataba huo walioingia ni wa awamu ya pili ambapo awamu ya kwanza TCB kupitia kupitia dhamana ya TADB ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 34.1 kwa wanufaika wa moja kwa moja 2,638 na wasio wa moja kwa moja zaidi ya 7,750 ambapo zaidi ya asilimia 95 walikua wakulima wadogo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege (wa pili kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Adam Mihayo (wa pili kuli), wakitia saini mkataba wa ushirikiano kwa ajili ya kutoa dhamana ya mikopo ya kilimo, mifugo na uvuvi. Na Mpigapicha Wetu

Anasema, TADB imefanya maboresho na imeongeza wigo wa dhamana kutoka asilimia 50 ya awali mpaka asilimia 70 kwa miradi ya wanawake, vijana na miradi ya mabadiliko ya tabia nchi ambapo pia itasaidia upatikanaji wa mikopo na kuchochea ongezeko la ajira kwa vijana.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Adam Mihayo anasema mkataba huo utaongeza wigo wa kutoa mikopo na kuwafikia wakulima wengi zaidi katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Anasema mikopo hiyo itawasaidia kuwapa mitaji itakayowawezesha kutoka kwenye kilimo cha kujikimu na kwenda kwenye kilimo cha biashara kwa riba nafuu ambapo pia itasasaidia kuinua uchumi wa nchi kwa ujumla.

“Tunaishukuru TADB kwa kutuongezea nguvu kwa ajili ya kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi wengi zaidi na mikopo hii itapatikana katika matawi yote ya TCB nchi nzima, nia ya kuongeza mikataba hii ni kuhakikisha tunawafikia wakulima wa pande zote za muungano kwa kuwaongezea mitaji kwa riba nafuu,” Anasema Mihayo.

Ushirikiano wa TCB na TADB umefanya jumla ya taasisi za kifedha zinazonufaika na mfuko wa dhamana wa wakulima wadogo (SCGS), kufikia 16 ambapo mpaka kufikia mwezi Disemba 2023, jumla ya mikopo ilikuwa Shilingi Bilioni 250.77 kwa wanufaika wa moja kwa moja zaidi ya 19,400 na ambao sio wa moja kwa moja zaidi ya 897,900 kutoa mikoa yote Tanzania bara na Visiwani.

TCB, zamani ikiitwa benki ya ya Posta (TPB), ni benki ya kwanza kuingia makubaliano na TADB tokea Mei 2018 na ni wanufaika wa kwanza wa mfuko wa dhamana wa wakulima wadogo kati ya benki zote washirika wa TADB.

Ushirikiano ta TCB unafanya jumla ya taasisi za kifedha zinazonufaika na mfuko wa dhamana wa wakulima wadogo (SCGS) kufikia 16.

Taasisi hizo zinajumuisha Benki za Biashara, Benki za Kijamii na Taasisi ndogo za kifedha (Microfinance Financial Institutions), zenye uwezo wa kuhudumia wakulima kupitia mtandao wao wa matawi zaidi ya 700 kote nchini.