Na Allan Vicent, Tabora
WAKULIMA wa kahawa zaidi ya 25,000 Mkoani Kigoma wameanza kunufaika na mbegu mpya za zao la kahawa iliyotafitiwa na Taasisi ya Utafiti wa zao la Kahawa hapa nchini (TACRI) na kuanza kusambazwa kwa wananchiwa mkoa huo.
Akiongea na Majira hili jana katika uwanja wa maonesho ya Nanenane wa Kanda ya Magharibi uliopo eneo la Ipuli Mkoani Tabora Meneja wa Taasisi hiyo Kanda ya Magharibi Twisege Andrew amesema kuwa matumizi ya mbegu mpya ya zao hilo yamehamasisha wananchi wengi zaidi kulima zao hilo.
Amesema kuwa awali kilimo hicho kilidorora hali iliyofanya wakulima wengi kukata tamaa lakini baada ya kuletewa mbegu mpya na kuhamasishwa kuzitumia, wakulima wameongezeka hadi kufikia 25,000 na katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 wameweza kuvuna zaidi ya tani 700 na kuziuza kwa zaidi ya sh bil 3.5.
Amesema kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na wataalamu wa taasisi hiyo kwa lengo la kuboresha kilimo cha kahawa katika mkoa huo ili kuleta tija kwa wakulima na kuinua uchumi wao.
“Tumenza mkakati wa kuhamasisha kilimo cha zao hilo katika Mkoa wa Tabora pia, kwa sasa tunaangalia maeneo yanayofaa katika halmashauri zoteza mkoa huo, ili kupanua wigo wa uzalishaji zao hilo katika mikoa yote ya kanda hiyo”, amesema.
Mtaalamu wa Utafiti wa Taasisi hiyo Peter Asenga alifafanua kuwa utafiti wao ulibaini aina 4 za mbegu bora aina ya robusta na aina 19 za arabika zinazofaa kwa kilimo hicho ambazo zina uwezo mkubwa wa kustahimili ukame, kuzaa matunda mengi, kukomaa kwa muda mfupi na kutopata magonjwa.
Alibainisha kuwa mbegu hizo zimekuwa mkombozi kwa wakulima kwani tangu zianze kutumika mavuno yameongezeka kutoka tani 1 kwa ekari hadi zaidi ya tani 2.3 kwa ekari moja.
Aliwataka kuendelea kuzingatia kanuni, taratibu na maelekezo ya wataalamu ili kuongeza uzalishaji na kunufaika zaidi na zao hilo.
Baadhi ya wakulima wa mkoa huo Thobias Kalimuwabu wa kijiji cha Kitambuka kata ya Mkatanga wilaya ya Buhigwe na Amos Kayage wa kijiji cha Nyalubada wilaya ya Kigoma vijijini walisema kuwa mbegu hiyo imewainua kimaisha kwani wengi wao sasa wamejenga nyumba bora na wanasomesha watoto wao.
More Stories
Baraza la wazee Kata ya Kilimani laahidi kampeni nyumba kwa nyumba
TMDA:Toeni taarifa za ufuatiliaji usalama wa vifaa tiba ,vitendanishi
The Desk & Chair yashusha neema Gereza la Butimba