Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
HALMASHAURI ya Manispaa Tabora imezindua mradi maalumu wa elimu, utakaohusisha ufyatuaji wa matofali zaidi ya 40,000 kwa lengo la kuboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari.
Akizindua mradi huo juzi, katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini, Komanya Kitwala amesema, mradi huo ni muhimu kwa kuwa utasaidia kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule zote.
Amesema, kuboreshwa kwa miundombinu hiyo kutaongeza hamasa kwa watoto kupenda shule hivyo kuchochea mahudhurio mazuri darasani na kuongeza ufaulu katika mitihani yao.
Kitwala amesema kwa kuanzia, manispaa imetenga mifuko 160 ya saruji kwa ajili ya mradi huo ambapo wanatarajia kupata matofali yasiyopungua 40,000, ambayo yatatumika kujenga vyumba vya madarasa na kumalizia maboma yaliyopo.
Ameongeza kuwa mradi huo, umelenga kumaliza tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu katika shule zote za manispaa hiyo na kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.
Alipongeza Watendaji na Maofisa Elimu Kata kwa kuhamasisha wananchi kuchangia maendeleo ya elimu katika maeneo yao, kwani hadi sasa juhudi hizo zimewezesha kujengwa maboma ya vyumba 16 vya madarasa na misingi 46.
“Tunataka tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa katika Halmashauri ya Manispaa Tabora libakie kuwa historia, naomba tushirikiane ili kuhakikisha miundombinu ya shule zetu zote inaboreshwa kwa kiasi kikubwa,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa, Bosco Ndunguru amesema, wamejipanga vizuri na atahakikisha mradi huo unafanikiwa kwa kiwango kikubwa, ili kuinua kiwango cha elimu katika manispaa hiyo.
Amewataka Watendaji wote wa vijiji na kata kutimiza wajibu wao ipasavyo na kuhakikisha maelekezo yote wanayopewa, wanayafanyia kazi kwa wakati ili kufanikisha mradi huu.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Ujenzi wa manispaa hiyo, Mwalimu Gaudensia Kafu amemshukuru Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kwa kuanzisha mradi huo, kwani utawezesha kujengwa kwa vyumba vya madarasa 40.
Ameahidi kusimamia ipasavyo utekelezaji wa mradi huo kuanzia mwanzo hadi mwisho, ili kuhakikisha lengo lililokusudiwa linafikiwa kwa asilimia 100 na kumaliza kabisa kero ya miundombinu ya shule zote katika manispaa hiyo.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango