November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tabora yapitisha Bajeti ya maendeleo ya zaidi ya Bil. 387

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MKOA wa Tabora umepitisha mapendekezo ya bajeti yake ya maendeleo ya kiasi cha sh bilioni 387.44 kwa ajili ya utekelezaji miradi ya wananchi kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025.

Bajeti hiyo imepitishwa jana na Wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) wakiwemo wadau wa maendeleo baada ya kuijadili kwa kina na kujiridhisha kuwa itachochea kasi ya maendeleo ya wakazi wa Halmashauri 8 za Mkoa huo.

Akiwasilisha rasimu ya bajeti hiyo Mchumi wa Mkoa Frederick Aron Ichwekeleza aliomba Kikao hicho kuidhinisha jumla ya sh bilioni 387.44 kwa ajili ya mipango ya maendeleo na matumizi ya kawaida ya Mkoa huo.

Alisema kuwa kati ya fedha hizo sh bilioni 346.37 ni fedha kutoka Serikali Kuu na sh bilioni 41.06 ni fedha za mapato ya ndani zitakayokusanywa na halmashauri zote 8 za Mkoa huo.

Alibainisha kuwa kiasi hicho cha fedha kimegawanywa katika mchanganuo wa aina tatu ambapo sh bil 229.68 ni kwa ajili ya mishahara, sh bil 42.84 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na sh bil 114.91 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

‘Makisio ya bajeti ya mwaka huu wa 2024/2025 ni sawa na ongezeko la asilimia 21 ya bajeti ya mwaka jana 2023/2024 ya kiasi cha sh bil 319.41, mwaka huu kuna ongezeko la bajeti ya mishahara, matumizi ya kawaida na maendeleo’, alisema.    

Mchumi Ichwekeleza alifafanua kuwa kati ya sh bil 114.91 zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, kiasi cha sh bil 72.41 ni fedha za ndani na sh bil 42.5 ni fedha za nje.

Aliongeza kuwa Sekretarieti ya Mkoa imeomba jumla ya sh bil 11.63 kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapo sh bilioni 3.77 ni za mishahara na sh bilioni 7.86 ni za matumizi mengineyo.

Kwa upande wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa, alisema wamekisia kukusanya na kutumia kiasi cha sh bilioni 260.89, kati ya hizo sh bilioni 225.91 ni za mishahara na sh bilioni 34.98 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC).

Aidha aliongeza kuwa Sekretarieti ya Mkoa imeomba kuidhinishiwa jumla ya sh bilioni 7.89 kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maendeleo ambapo sh bilioni 6.90 ni fedha za ndani na sh milioni 993.14 ni fedha za nje.

Wadau wa Maendeleo wa Mkoa wa Tabora wakifuatilia majadiliano ya Utekelezaji mipango ya maendeleo ya Mkoa huo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui Zakaria Mwansasu (katikati) akiongoza majadiliano ya mapendekezo ya bajeti ya Mkoa huo katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).