April 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi za uhifadhi zatakiwa kulinda maeneo ya hifadhi kwa teknolojia

Na Mwandishi wetu, Timesmajira, Arusha

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt.Pindi Chana (Mb) amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zinazojishughulisha na masuala ya uhifadhi kuhakikisha zinaweka mikakati ya kulinda maeneo ya hifadhi kwa teknolojia.

Ameyasema hayo jana Machi 29,2025 alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Arusha wakati wa ziara ya kikazi ambapo alikagua mradi wa Barabara ya kiwango cha changarawe (km 16) inayogharimu shilingi milioni 417.8 inayounganisha kata ya Ngarenanyuki na Usa River Wilaya ya Arumeru,Mkoani Arusha.

“Katika kukabiliana na ujangili na uvamizi katika maeneo ya hifadhi, wakati umefika wa kulinda maeneo yetu kwa kutumia teknolojia kama ndege nyuki ‘drones’, darubini, cctv cameras,” amesisitiza Chana.

Aidha, Chana ameipongeza menejimenti hiyo kwa utendaji kazi wake na ongezeko la mapato kutoka shilingi bilioni 6 mwaka 2019/2020 mpaka shilingi bilioni 9 mwaka 2023/ 2024 na ongezeko la watalii kutoka 57,697 hadi 81,761 kwa kipindi hicho.

“Nawapongeza na Mheshimiwa Rais anafurahishwa na shughuli za utalii zinazoendelea za ukusanyaji wa mapato” amesema Chana.

Katika hatua nyingine,Chana amesisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na mipango ya kuzuia na kupunguza takwimu za majeruhi ya wananchi kutokana na wanyamapori wakali.

Naye Kamishna Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Kuji ameahidi kutekeleza maelekezo yote na kuhakikisha anaboresha zaidi miundombinu ya hifadhi hiyo na kuongeza mapato zaidi.

Chana yupo Mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine atakagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utali.