December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya ZAYAMA kuwakomboa wakulima, wavuvi na wafugaji nchini

Na Jackline Martin, TimesMajira Online, DSM

Taasisi isiyo ya kiserikali inayosaidia wakulima, wafugaji na wavuvi iitwayo Zayama Foundation imeandaa semina na wanakijiji wa Mvuti, Kata ya Msongola, Wilaya ya Ilala Dar Es Salaam ili kuwapa elimu kuhusu kilimo, ufugaji na uvuvi.

Dina Sudi anbaye ni Katibu wa Taasisi ya ZAYAMA Foundation akikabidhi miche tayari kwaajili ya kupandwa

Akizungumza na Gazeti la Majira wakati wa semina hiyo Zaituni Biboze Mwenyekiti wa Zayama Foundation alisema Zayama ipo kuwasaidia wajasiriamali ili kupata bidhaa Bora na zenye tija;

“Lengo letu ni kusaidia wakulima, wafugaji na wavuvi ili wafike mbali kwa kupata bidhaa bora, zenye kiwango na kupata masoko sehemu mbali mbali hata nje ya nchi.” Alisema Zaituni

Aidha Zaituni aliwataka wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza ili kupata elimu sahihi kuhusu kilimo, ufugaji na uvuvi

Naye Katibu wa Taasisi hiyo, Dina Sudi Mwakagenda alisema, Zayama imejikita kufanya kilimo, ufugaji na uvuvi vionekane kuwa chanzo cha mapato na kuhakikisha inatimiza malengo na mwanachama kwa manufaa.

Maofisa wa ZAYAMA (waliovaa fulana za bluu) wakiwa katika picha ya pamoja na Wanakijiji wa Mvuti baada ya mafunzo yaliyotolewa kijijini hapo mwishoni mwa wiki.

“Tunataka kuwainua wanachama wetu na kuwezesha kukua, kikubwa mwananchama anachopata kutoka kwetu ni elimu, vitendea kazi na kuuungwa mkono ili kuendelea na kupata masoko” Alisema Dina

Kwa upande wake Afisa Masoko wa ZAYAMA Foundation, Endru Sudy Andrea alisema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mapokeo ni makubwa na taasisi hiyo inatarajia kupokea wajasiriamali wengi zaidi.

“Muelekeo wa taasisi ni mkubwa, mwitikio ni mzuri kutokana na utendaji kazi wetu, watu wanajitokeza kwa wingi kuungana nasi, hukut tukijitahidi kuwahudumia na kutimiza yale tunayo ahidi” Alisema Andrew

Mpaka sasa ZAYAMA imeshatembelea na kutoa huduma katika wilaya mbili ambapo ilianzia Wilaya ya Kigamboni na kwa sasa Ilala huku wakiongeza nguvu kutokana na mahitaji ya walengwa.

Afisa Masoko huyo aliahidi elimu ambayo itatengeneza msingi utakaoleta mapinduzi katika soko kwa kuzalisha bidhaa zenye viwango ili kuleta mapinduzi katika soko.

ZAYAMA imejitahidi kuwafikia wajasiriamali na kuwapa elimu ili kuwawezesha kuzipa ubora bidhaa wanazozalisha ili ziweze kuuzika. Kwa mujibu wa Selemani Rajabu ambaye ni PDS wa ZAYAMA Foundation, taasisi hiyo inawafikia na kuwapa elimu kwa kuwafuata wazalishaji ambao na kuwasimamia kuanzia katika kitalu shambani hadi kufikisha mazao sokoni.

Selemani ally akiwa amebeba pampu ya kumwagilia mbogamboga aliyokabidhiwa na Taasisi isiyo ya kiserikali inayosaidia wakulima, wafugaji na wavuvi  (ZAYAMA Foundation) kutokana na juhudi nzuri katika kilimo, zawadi hiyo imetolewa katika semina iliyoendeshwa na taasisi hiyo katika Kijiji Cha Mvuti, Kata ya Msongola, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam. Wengine ni maofisa kutoka ZAYAMA Foundation, kuanzia kushoto ni Dina Sudy (Katibu wa Taasisi hiyo), Mohamed Ally (Meneja Rasilimali Watu), Rajabu Selemani (PDS), pamoja na Sharifa Msheni. Picha na Prosper Rutayuga, TimesMajira Online.

“Bidhaa ya mkulima ikishafika sokoni tunatafuta namna ya kuifanya iweze kuuzika” anasema Rajabu na kuongeza kuwa kwa wale ambao wameshapata elimu ya kilimo na ufugaji, mapokeo yao ni mazuri

Selemani aliongeza “kwasababu hatumpi tu bidhaa bali tunampa na elimu sahihi hivyo hatuwatupi bali tunawasimamia kutoka hatua moja hadi nyingine”

(JINA) Meneja Rasimali watu kutoka taaissi hiyo amesema wanatoa misaada mbalimbali kwa wajasiriamali lakini pia wanawapa na mikopo ili kuwainua wakulima Tanzania;

“Zayama inatoa misaada kwa wakulima, wafugaji na wavuvi na msaada mkubwa kabisa ambao ni elimu. Pia tunawapa pembejeo, mbegu, vifaranga na hata kutoa mikopo katika sekta zote tatu.”

Amasema kuwa mikopo inaendana na mtu anachokifanya, mfano maofisa wa taasisi huyo huangalia mkulima analima mazao gani mahitaji yake

Meneja huyo amefafanua kuwa mikopo hiyo haina riba kwani lengo ni kumsaidia mkulima kupambana na changamoto ikiwa ni pamoja na mtaji, nyakati nyingine hutoa vitendea kazi badala ya fedha taslimu kutegemea na mahitaji ya mkulima.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mvuti (JINA), aliwashukuru ZAYAMA kwa kufika na kutoa elimu kwani italeta manufaa makubwa kwa wakazi wa Kijiji hicho.

Amsema “Semina iliyoendeshwa na ZAYAMA ni kitu tumekuwa tukikisubiri kwa hamu ambapo leo imetufikia na kupata fursa ya kujua ni nini tunahitaji katika kilimo, ufugaji na uvuvi”

Taasisi ya Zayama ilianzishwa rasmi tarehe 18/3/2021 kwa lengo la kusaidia kupambana na changamoto wanazokutana nazo wakulima, wavuvi na wafugaji ambazo zinaweza kugeuzwa kuwa fursa.