January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya utafiti zao la kahawa kuanza uzalishaji wa miche ya kahawa kwa miaka mitano ijayo

Na Esther Macha,Timesmajira Online, Mbeya

TAASISI ya Utafiti wa zao  Kahawa Tanzania (TaCRI) imejipanga kuzalisha  tani 3000 za miche ya kahawa katika kipindi cha miaka mitano ijayo kwa kuzingatia ubora na uwezo wa mkulima kupata mavuno mengi.

Akizungumza na gazeti hili jana Meneja wa Utafiti zao la Kahawa  Tanzania, (TaCRI) Nyanda za Juu kusini Kanda ya Mbeya, Dismas Pangalasi, amesema  kuwa  uzalishaji wa miche hiyo utaanza katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2022.

Pangalasi amesema  kuwa mikakati ya taasisi hiyo  ni kuweza kukuza sekta ya kilimo  cha kahawa Nchini .

Hata hivyo Meneja huyo amesema kuwa uzalishaji wa miche  hiyo pia watahakikisha  wanazingatia  uwezo wa kukinzana na magonjwa mbalimbali ambayo yanashambulia mimea ya zao hilo la kahawa.

“Licha ya mikakati ya Taasisi hii, kuwasaidia wakulima lakini bado tunakabiliwa na mahitaji makubwa  ya miche ya kisasa kwa wakulima ukilinganisha uzalishaji wenyewe  ambapo kwa sasa ni tani milioni tatu na mahitaji yakiwa ni milioni 18 kwa Kanda ya Mbeya,” alisema Pangalasi.

Aidha  kuna tatizo la baadhi ya wakulima na  wadau kutokujua umuhimu wa kufanya utafiti wa afya ya udongo licha ya kupeleka miche kwa wakulima hivyo kuchangia mavuno kutokuwa bora na mengi.

Kutokana na hali hiyo, ametoa  hamasa wakulima pamoja na wadau wengine wanaohusika na mnyororo wa thamani wa zao la kahawa kuhamasishana kupima afya ya udongo  ili kujua mbegu gani inapaswa kutumika katika kulingana na kila eneo.

Kwa upande wake, Meneja wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la Cafe Africa Tanzania, Dafrosa Sanga amesema miongoni mwa majukumu ya shirika hilo ni kuwahamasisha wakulima upandaji wa miche bora ya kahawa ili kupata mavuno mengi.

Amesema katika jukwaa la wakulima pamoja na wadau wanaohusika kwenye mnyororo wa thamani wa zao la kahawa,  kunatoa fursa ya kujadili kwa pamoja namna ambayo itasaidia kukidhi mahitaji ya miche kwa wakulima ili waongeze uzalishaji na kulima mimea ambayo itatoa mavuno bora ambayo yatakadhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.