March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya Uongozi kuja na programu  mpya ya viongozi Chipukizi

Na Penina Malundo,Timesmajira

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi ,Kadari Singo amesema  Taasisi ya Uongozi inatarajia kuanzisha programu nyingine mpya ya Viongozi Chipukizi ambayo itaanza kuwaandaa viongozi mapema.

Ameyasema hayo juzi Jijini Dar es Salaam,Singo amesema programu hiyo itawasaidia viongozi hao wakiwa wachanga ili wanapokuja kushika nafasi waweze kutumikia vema.

Amesema wakati mwingine viongozi wanalewa madaraka kwa sababu wanakuwa wamepewa nguvu na sio ujuzi,matokeo yake wanatumia nguvu na sio ujuzi walioupata katika mafunzo kama haya.

”Hili Jukwaa la wahitimu waliomaliza mafunzo ya uongozi watakuwa sehemu yakuwajengea uwezo hawa chipukizi,ambapo utakuwa ni mfumo ambao wale waliotangulia wawe wanawaongoza viongozi hao chipukizi,”amesema

Singo amesisitiza kuwa Jukwaa hili sio la taasisi bali ni la wanajumuiya wenyewe ila kwa kuanza litakuwa linawakutanisha wahitimu hao kwa mwaka mara moja kwa lengo la kubadilishana uzoefu.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Uongozi,Ombeni Sefue amesema mafanikio hayo yote ya Taasisi ya Uongozi yametokana na msaada wa wazi na endelevu kutoka kwa Serikali ya Tanzania na Finland.