April 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya Tulia Trust yamfuta machozi bibi anayeishi kwa kuokota makopo

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

Mjane Eva Chungu (70) Mkazi wa Mtaa wa Mwanyanje kata ya Igawilo ambaye anaishi  kwa kuokota makopo na mabaki ya mikaa sokoni amefutwa machozi na Taasisi ya Tulia Trust baada ya kuanza hatua ya kumjengea ya nyumba ya kuishi.

Taasisi hiyo inajenga nyumba tatu katika kata tofauti ikiwewo ya Mjane Eva  kutokana na makazi yake ya awali kuwa hatarishi kwa maisha yake.

Aprili 5,2025 wakati Taasisi ya Trust ilipofika nyumbani kwa Chungu kwa ajili kuanza ujenzi wa nyumba yake ameeleza kuwa alikuwa anabeba mabaki sokoni na kuokota makopo na kuuza ili apate fedha za kujikwamua kiuchumi kwa ajili ya kununua mahitaji.

Chungu amesema mbali na changamoto mbalimbali alizopitia aliamua kufyatua tofari na kujenga nyumba ambayo imebomolewa na kujengwa nyingine kufuatia mazingira yake kutokuwa rafiki.

Joshua Mwakanolo ni Afisa Habari wa Taasisi ya Tulia Trust amesema kuwa ujenzi wa nyumba hizo tatu wahitaji watatu wa mitaa ya Gombe kusini kata itezi ,mtaa wa utukuyu kata ya Uyole pamoja na mtaa wa Mwanjanje kata ya Igawilo ambazo zinategemewa kukamilika ndani ya mwezi mmoja ili ziweze kukabidhiwa kwa wahitaji hao walioibuliwa wakati wa mbio za bendera ya upendo inayoratibiwa na Taasisi hiyo chini ya Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini Dkt.Tulia Ackson.

“Mkurugenzi wetu ametoa maelekezo kuhakikisha nyumba zote tatu za  wahitaji zinakamilika ndani ya  mwezi mmoja ili wahitaji hawa waweze kukabidhiwa mapema iwezekanavyo hivyo tutegemee Dkt.Tulia mwenyewe mwezi Mei,mwaka huu atakuja kukabidhi nyumba hizi ambazo idadi yake itakua imefikia 21 kujengwa ndani ya mkoa wa Mbeya na nje ya mkoa wa Mbeya amesema  Mwakanolo.

Aidha Mwakanolo amesema kuwa mpaka sasa nyumba 18, zimejengwa na kukabidhiwa kwa walengwa na kuwa siku ya hiyo kupitia bendera ya upendo kwa siku kadhaa zilizopita ambayo ilikimbikizwa kata ya Uyole, Igawilo  na Itezi  baada ya kukimbiza bendera hiyo waliweza kutoa vyakula,mavazi, mahitaji ya shule na wanafunzi walioshindwa kuendelea na  masomo ambapo Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini aliagiza  kuhakikisha wanahudumiwa vizuri katika kupata mahitaji yote ya msingi.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwanjanje, Joseph Ndambo amesema kuwa  mama huyo  alipatikana  wakati  bendera ya upendo ilipopita mitaa minne ya kata ya Igawilo na baada ya kufanya tahlthimi kamati ya maendeleo ya kata ilimptisha mama huyo ili aweze kujengewa nyumba na kupongeza jitihada kubwa za Mbunge wa Jimbo hilo Dkt.Tulia Ackson katika kuona kundi la wahitaji.

Rhoda chengula amesema kuwa mara ya kwanza kumuona bibi huyo alimuona akiokota makopo kwenye maahimo ya kutupa taka ili aweze kuuza na kumsaidia kununua chakula lakini pia  mazingira ya kuishi peke yake yalisababisha vijana kumwingilia usiku na kumbaka.

Jirani mwingine ,Emmanuel Njowele amesema kama majirani walikuwa wa kwanza kutoka kumwangalia  bibi huyo  kwani amekuwa akiishi maisha duni hivyo kushukuru Taasisi ya Tulia Trust chini ya Mkurugenzi wake Dkt Tulia Ackson kwa ujenzi wa nyumba hiyo imekuwa mkombozi kwake.

“Kwakweli tunasema Dkt.Tulia Mungu ambariki kwa msaada huu wa ujenzi wa nyumba tunaomba msichoke na kusaidia wengine wenye uhitaji kama wa huyu bibi,” amesema Njowele.