May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya Nelson Mandela yaeleza utekelezaji na vipaumbele vyake 2022/23

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,  Dodoma.

TAASISI ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela imesema kwa mwaka 2022/23, Serikali imeidhinisha bajeti ya takriban Shilingi bilioni 43 kwa ajili ya kukamirisha miradi ya Taasisi hiyo.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo na  Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela,Prof.Emmanuel Luoga wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji na vipaumbele vya Taasisi hiyo kwa mwaka 2022/23.

Luoga ametaja vipambaumbele hivyo kuwa ni Ujenzi wa bweni maalum kwa ajili ya wanachuo wanawake wenye mahitaji maalum na wenye watoto wadogo ni mradi ambao tayari umeshaanza tangu Oktoba, 2021 na kiasi cha Shilingi bilioni 1.7 kimeshatumika.

“Ujenzi huu utafanyika kwa awamu tatu, awamu ya kwanza ambayo itachukua wanafunzi 180 imekadiriwa kutumia Shilingi bilioni 4.8 na inatarajiwa kukamilika Juni, 2023 huku Ujenzi wake umefikia asilimia 43,”amesema.

Kipaumbele kingine ni Taasisi hiyo inajikita katika matumizi ya TEHAMA ambapo itapata Dola za Marekani milioni 10 mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia, fedha hiyo itatumika kuimarisha mifumo ya TEHAMA na kuhakikisha tunapata ithibati ya maabara yetu kufikia viwango vya kimataifa.

“Maabara yetu itakapokamilika na kupata ithibati itakuwa ni moja ya maabara itakayotusaidia kuhakikisha bidhaa zetu zinapata soko popote duniani,”amesema.

Pia amesema Taasisi hiyo imejikita katika kuboresha ufundishaji kwa kutumia teknolojia ya masafa (e-learning) kwa waadhiri na kupanua wigo kwa wanafunzi walio mbali na kampasi kupata elimu ya masafa.

“Katika masuala ya utafiti na ubunifu, mpaka sasa taasisi hii imefanikiwa kufanya bunifu 73 ambazo ni matokeo ya ushirikiano wa hali ya juu kati ya wahadhiri na wanafunzi pamoja na Serikali na wadau wa maendeleo kutoka nje ya nchi,

“Taasisi yetu kwa kushirikiana na taasisi zingine mbili tunaanzisha Kituo cha Umahiri cha Ndizi ambacho kitahusika na masuala ya utafiti wa mbegu, namna ya kuongeza tija katika upandaji na usimamizi wa zao la ndizi na matumizi bora.

Hata hivyo amesema kuwa inazidi kuongeza ushirikiano kati ya taasisi hiyo na zingine ndani na nje ya nchi katika Kanda ya Afrika Mashariki na Taasisi za Kimataifa,tumejipanga kuongeza mashirikiano na taasisi zinazohusu fedha, biashara, viwanda hasa taasisi za Sekta Binafsi.

Pamoja na hayo Prof.Luoga alitaja manufaa ya Taasisi hiyo kwa wananchi kwa Taifa ambapo alisema kuwa Taasisi hiyo imesaidia kuongeza wataalam na wabunifu nchini, imekuwa ni mwalimu wa walimu kwa sababu walimu wengi nchini na Afrika Mashariki ambao wanafundisha masuala ya sayansi wamefundishwa katika taasisi hii.

Alisema kuwa Taasisi hiyo inafanya tafiti nyingi za kuzalisha viuatilifu asilia ili kupambana na magonjwa ya mimea, hivyo kuongeza tija katika kilimo.

“Tumeendelea kubuni majiko sanifu yanayopunguza gharama ambayo yanatumia gesi na nishati zingine mbadala pia Taasisi inahusika katika kuchakata majitaka ili kuzuia uharibifu wa mazingira, tayari kuna tafiti zinazoendelea na zingine zinafanya kazi kuchakata majitaka ambayo yanaweza kutumika kwa matumizi mengine,”alisema.

Aidha amesema kuwa Kuelekea miaka 61 ya Uhuru, Taasisi imejikita katika kufahamika na kufahamu filosofia ya chuo kutoka hatua tatu za kufundisha, kufanya utafiti na uenezi kwenda kwenye hatua tano kwa kuongeza masuala ya uatamizi na ubiasharishaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ametoa rai kwa vyuo mbalimbali nchini kuweka kozi za umahiri kwa Waandishi wa Habari ili wakafanye tafiti za kutosha, hivyo kuondokana na kutoa habari za uongo na zisizokuwa na tija kwa umma.

Amesema kuwa Serikali inatambua kwamba bila sayansi hakuna maendeleo, mageuzi wala mapinduzi yoyote ya kiuchumi, hivyo tunataka tutumie sayansi kama moja ya nguzo zitakazotuvusha kwenda kwenye maendeleo zaidi.

“Chuo hiki ni cha kitaaluma lakini mwelekeo wake ni kufanya kazi kubwa ya kuunganisha kati ya wanataaluma na jamii ndio maana kimejikita zaidi katika tafiti, hili ni eneo muhimu ambalo nchi yetu inalihitaji,”amesema.

Amesema kuwa Serikali inafanya kazi kubwa kuandaa wanasayansi kutoka shule za msingi mpaka shahada za kwanza, kwa sasa Serikali inajenga shule moja ya sekondari ya masomo ya sayansi kwa kila mkoa kwa ajili ya wasichana.