December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya Marie Stopes Tanzania, waongeza wigo kwa upande wa wataalamu

Judith Ferdinand, Mwanza

Katika kuunga mkono jitihada za serikali upande wa utoaji huduma za afya, taasisi ya Marie Stopes Tanzania,
wameongeza wigo kwa upande wa wataalamu ambapo wanategemea uwepo wa daktari bingwa wa watoto na daktari bingwa wa akina mama.

Huku mpaka sasa wana zahanati 9 katika mikoa ya Unguja Zanzibar, Musoma, Kahama, Mwanza, Mbeya, Iringa, Kimara, Arusha na hivi karibuni watafungua Makambako, na hospitali ya mama na mtoto iliyopo Mwenge Mkoa wa Dar es salaam.

Hayo yamebainishwa na Msimamizi wa vituo na hospitali za Marie Stopes Tanzania Dkt. Emanuel Kimario, wakati akizindua kituo cha taasisi ya Marie Stopes Tanzania ambacho awali kilikuwa Nyegezi wilayani Nyamaganana sasa kimehamishiwa mtaa Ghana wilayani Ilemela.

Dkt. Kimario amesema wanaunga mkono juhudi za serikali za kuwafikishia wananchi huduma ambapo licha ya kuendelea kutoa huduma zote pia wameongeza wigo kwa upande wa wataalamu ambapo wanategemea uwepo wa daktari bingwa wa watoto na daktari bingwa wa akina mama.

Amesema huduma nyingine zinazotolewa ni huduma za afya ya uzazi, afya kwa ujumla, kliniki kwa akina mama na watoto vipimo vya ‘ultrasound’ na maabara, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matibabu ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi, pamoja na chanjo na uchunguzi wa homa ya ini.

Sanjari na hayo amesema, katika kipindi hiki cha ufunguzi wametoa ofa kwa wateja kwa kutoa huduma mbalimbali bila malipo ikiwemo huduma za afya ya uzazi ikiwemo njia za afya ya uzazi, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti, upimaji wa VVU kwa hiari, pamoja na kupata ushauri wa daktari.

Aidha aliishukuru serikali kwa kuendelea kuwa bega kwa bega nao ili kuhakikisha wanawafikia wananchi wa Mwanza na watanzania kwa kutoa elimu na huduma za afya kwa ujumla.

Kwa upande wake
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Nyagani Finias
amewasisitiza wananchi kutumia fursa
ya upimaji wa afya na huduma za kiafya zinazotolewa bure na taasisi ya Marie Stopes Tanzania kuanzia tarehe 15 hadi 19 mwezi Novemba mwaka huu.

“Tuitumie fursa ya siku hizo vizuri na baada ya hapo tuendelee kupata huduma na kupiga simu ya bure kwa namba zilizotolewa na kituo kwa ajili ya kuweka miadi lini uweze kuonana na daktari kulingana na ratiba yake,” amesema Finias.

Aliongeza kuwa kuhama kwa kituo hicho kutoka Wilaya ya Nyamagana kwenda Ilemela kunaongeza idadi ya vituo vya afya kutoka vituo 63 na kufika vituo 64 na kati ya hivyo vituo 19 ni vya serikali.

Naye Meneja wa Mawasiliano wa taasisi ya Marie Stopes Tanzania,Esther Shedafa amesema wamehama kutoka Nyegezi na kwenda katikati ya jiji ili kuwafikia wateja na watanzania wote kwa ajili ya huduma za afya kwa urahisi zaidi.

Pia amesema wameongeza wigo kwa kuwa na kituo cha mawasiliano kinachotoa huduma bure.

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Nyagani Finias akikata utepe ishara ya kuzindua kituo cha Taasisi ya Marie Stopes Tanzania kilichoamishiwa mtaa wa Ghana wilayani Ilemela kutoka Nyegezi wilayani Nyamagana, kulia ni Msimamizi wa vituo na hospitali ya Marie Stopes Tanzania Dkt. Emanuel Kimario.picha na Judith Ferdinand.

Clinical Officer wa Marie Stopes Tanzania Dkt.Leocadia Juma akitoa huduma kwa mteja Anna-Joyce Nishange mkazi wa jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa kituo cha taasisi hiyo kilichopo mtaa wa Ghana wilayani Ilemela.picha na Judith Ferdinand.

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Nyagani Finias akikata keki wakati akizindua kituo cha taasisi ya Marie Stopes Tanzania kilichoamishiwa mtaa wa Ghana wilayani Ilemela kutoka Nyegezi wilayani Nyamagana.picha na Judith Ferdinand.