December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya Liberty Sparks yawakutanisha pamoja wanafunzi wa vyuo kujifunza Uchumi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Taasisi ya Liberty Sparks imewakutanisha pamoja wanafunzi kutoka vyuo tofauti nchini ili kujifunza zaidi juu ya masuala ya kiuchumi na maendeleo, kutoka kwa wataalamu na manguli wa uchumi katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa-Posta Tanzania.

Kongamano hili la wanafunzi maarufu kama (UHURU CON) hukutana kila mwaka na sasa ni mara ya sita limekuwa likiwawezesha wanafunzi na vijana kukutana, kujifunza, kujadili na kubadilishana mawazo juu ya mifumo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii itakayowawezesha kupambana na changamoto katika jamii zao.

Wazungumzaji wa Mwaka huu ilijumusiha Maprofesa na Wakufunzi wa uchumi kutoka ndani na nje ya nchi.


Katika kongamano hili, vijana na wadau walijifunza zaidi namna biashara za mipakani zinavyoweza kustawisha maisha ya wafanyabiashara na wananchi.

Kama vikwazo visivyo vya kikodi vitaisha, fursa za masoko zitaongezeka na hali ya maisha itaimarika kwasababu wananchi watakuwa na uhuru wa kuchagua bidhaa wanazozitaka kwa bei nafuu, alisema Mkurugenzi wa Liberty Sparks.

Wajibu wa vyombo vya habari katika kuchochea mapinduzi ya kibiashara nao haukusahaulika. John Leask, alisema kuwa ukuaji wa biashara unategemea sana wafanyabiashara wenye maarifa na taarifa sahihi za kibiashara.

Alifafanua jinsi vyombo vya habari vilivyoisaidia nchi kama Marekani kupiga hatua kiuchumi kwa kusambaza elimu ya soko huria ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kulinda maslahi ya wananchi na serikali yao.

Pia aliwaasa vijana kupunguza muda wa kufuatialia mambo yasiyo na ulazima ili kupata muda wakutosha katika kufanyia kazi mawazo na mbinu za kukabiliana na umasikini nchini.
Li Schooland alifafanua vyema kuhusu mfumo wa China kiuchumi.

Alisema kwamba, Katika miaka ya 1950 China ilikuwa maskini kuliko nchi yoyote Afrika.

Wakati huo serikali ya China ilikuwa na ufisadi mwingi huku wananchi wake wakiangamia kwa umaskini. Mabadiliko ya kiuchumi China, yalichochewa na ujio wa mifumo ya soko huria baada ya Mmao Tse Tung kushika madaraka.
Hata nchi nyingine zinaweza kujifunza kwa China, alisema.

Katika hili, Professa Ken, aliongezea kuwa soko huria linasaidia kutatua changamoto nyingi ikiwapo mifumo na gunduzi za tekinoloji zinazosaidia katika kupunguza vifo na na kuongeza umri wa kuishi, kuchochea ushindani wa kibiashara, upatikanaji wa bidhaa nafuu, kuchochea uhuru wa kisiasa, kushusha umasikini na ufisadi katika nchi. Profesa Ken aliongezea kuwa, soko huria na uhamiaji haviwezi kutenganishwa kwa sababu uhamiaji huchochea ushindani, ubunifu, maendeleo ya teknolojia, mabadilishano ya ujuzi na maarifa katika soko.

Mengine yaliyosisitizwa katika Kongamano ni pamoja na watu kufanya kazi kwa bidii, kuwa wavumlivu na wabunifu katika uzalishaji mali, utafutaji pesa, kupunguza matumizi, na usimamizi wa malengo. Carlyle Rogers aliyasema haya huku akiikumbusha serikali kuweka viwango rafiki ili kuweza kupata mapato bila kuathiri ukuaji wa kibiashara na maendeleo ya watu.

Baadhi ya washiriki walielezea namna kodi kubwa inavyoweza kuua au kuchochea maendeleo kama msemaji Daniel Mitchell alivyosema kuwa “Kadri kodi inavyokuwa juu, ndivyo maendeleo yanavyoshuka”.

Naye mshiriki Maliea Mboje alisema kuwa, sheria na kanuni zisizorafiki ni changamoto kubwa linalopelekea ukosefu wa ajira, na gharama kubwa za uanzishaji makampuni na uanzishaji biashara. Aliongezea kuwa hatua za kufuata bado ni changamoto na ni kitu kinachowakwamisha wahitimu wengi wa vyuo vikuu kujiajiri, Malieta aliiomba serikali kuendelea kurahisisha mazingira ya uanzishaji na ufanyaji biashara nchini.

Mategemeo ya Liberty Sparks ni kuona kuwa taasisi za kiserikali, vijana na wadau wa maendeleo wanaunga mkono juhudi za zakuboresha mazingira ya ufanyaji biashara Tanzania. Aliyasema haya wakati akitoa matokeo ya utafiti na kampeni ya Ujirani Mwema iliyofanywa na Dokta Sauti Magai katika kuboresha biashara za mipakani, nchini Tanzania.

Mkurugenzi wa Liberty Sparks, Evans Exaud aliongezea kuwa, bado kuna watanzania maskini na umaskini utashuka kama tutakubali kuwekeza kwenye mifumo itakayorahisisha biashara za mipakani hasa kwenye uingiziaji na utumaji wa bidhaa nje ya nchini.