June 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya Jalaram Seva Mandal yatoa msaada kwa Watanzania

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

TAASISI ya Jalaram Seva Mandal imetoa msaada wa matibabu ya Upasuaji wa wagonjwa takribani 33 wenye magonjwa mbalimbali ikiwemo Ngirimaji,Henia pamoja na Tezi Dume kwa wagonjwa wanaume huku wanawake wakisaidiwa katika uzibuaji wa mirija ya uzazi ambayo imekuwa ikiwatesa wanawake wengi kukosa watoto.

Miongoni mwa wagonjwa hao wametoka katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Morogoro,Dar es Salaam pamoja na Pwani ambao wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa hayo kwa kipindi cha miaka mingi.

Akizungumza awali na wagonjwa hao juzi jijini Dar es Salaam,Naibu Spika wa Bunge,Mussa Azzan Zungu alisema taasisi hiyo imekuwa na kawaida ya kusaidia watu mbalimbali hususan wale wenye matatizo ya upasuaji na kipato chao ni kidogo.

Amesema Taasisi hiyo inaunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuhudumia wananchi wa Tanzania kwani hii ni zaidi ya mara 25 yeye kufika katika Taasisi hiyo na kukabidhi risiti za wagonjwa kwenda kufanyiwa matibabu.

”Tunawashukuru sana wadau hawa,wagonjwa hawa leo wanapewa fomu maalum ambazo zitawaruhusu kwenda kufanya uchunguzi na gharama ya kwenda kufanyiwa uchunguzi na matibabu zinakuwa juu ya Taasisi hiyo.

”Hizi ni jitihada za kuunga mkono Serikali yetu kusaidia wananchi ambao wanachangamoto ya matibabu na uwezo wa kipato kwao ni mdogo,”amesema.

Amesema kuwa wanaipongeza taasisi hiyo kwa kuwa sehemu ya kusaidia jamii na kuhakikisha inakuwa salama kwani Rais Samia ameweza kuboresha vituo vingi vya afya vya kila wilaya lengo ikiwa ni kuwafikia wananchi wa maeneo mbalimbali.

Zungu alitoa wito kwa jamii kuwa na kawaida ya kusaidia na kuchangia watu wenye mahitaji kwani ni jambo la faraja.”Ukibarikiwa na kipato kitoe umsaidie mwenzio kila unapotoa Mungu anakurudishia mara tatu,kama hii Taasisi inavyofanya na ndo maana wapo zaidi ya miaka 60 sasa nchini,”amesema

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Kishor Modi amesema taasisi yao ipo kwa miaka mingi nchini imekuwa ikitoa misaada kwa watu wenye ulemavu na wagonjwa wanaosumbuliwa magonjwa mbalimbali ikiwemo henia,ngilimaji,tezi dume na mirija ya uzazi kuziba kwa wanawake.

”Tumepokea wagonjwa takribani 33 ambao matibabu yao yatagharimu kiasi cha sh. Milioni 40,awali tulifanya zoezi kama hili kwa miezi mitatu nyuma ambapo kulikuwa na wagonjwa wapatao 37 waliogharimu kiasi cha sh.Milioni 51.

”Kwasasa changamoto tuliyonayo ni kuomba watu binafsi kutusaidia katika kuwasadia wagonjwa hao kwani gharama hiyo ni kubwa na kuna watoto wakinamama na wakinababa,”amesisitiza.

Naye Mmoja wa wagonjwa waliopatiwa Msaada huo,Hasaan Maulid Mkazi wa Buguruni ameiishukuru taasisi hiyo kwa kuwa na moyo wa kujitoa kwa watanzania kwani wamekuwa msaada mkubwa kwa watu wenye vipato vya chini.

”Nashukuru sisi wenye kipato cha chini kupata msaada huu kwa maana sisi wenyewe tusingeweza kupata matibabu haya kutokana na vipato vyetu,tunawashukuru sana Mungu awasaidie kwa kuwapa imani ya kuwasaidia wengine.

”Kwani tatizo langu linazaidi ya miaka 10 lakini kutokana uwezo wangu wakipato nikashindwa kujitibu kiharaka hivyo baada ya kupata msaada huu nawashukuru sana hii Taasisi,”amesema.