November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya AKRDF, MUHAS waadhimisha siku ya magonjwa adimu

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

WATABIBU mbalimbali nchi wamesisitiza jamii kutoa msaada kwa wagonjwa wanaokabiliwa na magonjwa adimu pamoja na kusisitiza umuhimu wa kuwekeza katika utafiti ili kuboresha huduma kwa idadi hii ya watu walio hatarini.

Watabibu hao walitoa wito huo wakati wa maadhimisho ya siku ya magonjwa adimu Duniani ambayo huadhimishwa kila mwisho wa Mwezi Februari kila Mwaka ambapo kwa Mwaka huu yaliadhimishwa katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Daktari Edward Kija, alisema Tanzania inakabiliwa na pengo kubwa la ukusanyaji wa takwimu zinazohusiana na magonjwa adimu.

“Wakati taifa letu linakabiliwa na pengo katika ukusanyaji wa takwimu zinazohusiana na magonjwa adimu na kuacha kuzungumzia muhimu wa jamii kupata uelewa kuhusu magonjwa hayo ndio magonjwa hayo yanavyozidi kupata nafasi ya kusababisha kifo,” alielezea.

Hata hivyo, Dk Kija alitoa wito kwa jamii ya Watanzania kuwaunga mkono watu wanaokabiliwa na magonjwa adimu ambapo aliangazia changamoto ambazo mara nyingi hazizingatiwi ambazo watu na familia zao hukutana nazo kwa sababu ya uelewa mdogo bila ya kuwa na usaidizi.

“Msaada wa pamoja wa jamii ni muhimu katika kujenga mazingira ambapo wale walio na magonjwa adimu wanahisi kueleweka, kutunzwa, na kuwezeshwa,” alisema.

Kwa upande wake, Profesa Bruno Sunguya ambaye ni Profesa Mshiriki wa Lishe ya Afya ya Jamii, Naibu Makamu Mkuu wa Utafiti na Ushauri wa MUHAS alikiri kutokuwepo kwa takwimu za kina za magonjwa adimu nchini Tanzania.

Profesa Bruno alisisitiza mapungufu katika ukusanyaji wa data na juhudi za utafiti zinazohusiana na magonjwa adimu.

“Bila taarifa sahihi, inakuwa changamoto kwa wataalamu wa afya kurekebisha afua na kutenga rasilimali kwa ufanisi,” alisema.

Profesa Bruno alisema kuwa tayari mipango iko mbioni kufanya tafiti kwa ushirikiano na vyuo vingine ili kubaini chanzo halisi na tiba sahihi.

Alisema kuwa majibu ya tafiti yatatupa majibu kwa matatizo yaliyopo na kutoa ushauri wa kisera na miongozo ya kufuatwa.

“Tunaahidi kuhakikisha tafiti zetu zinaleta matokeo ya majibu kwa magonjwa adimu ili kubaini na kupata tiba sahihi magonjwa haya,”alisema.

Naye Daktari Bingwa wa magonjwa ya watoto, Professa Karim Manji, alisema kuwa uelewa kwa jamii ni muhimu kuepusha unyanyapaa kwa wagonjwa.

Alisema kuwa watoto wengine wanaozaliwa na tatizo hili hawapati tiba sahihi na hivyo kufariki wengine wakihofia unyanyapaa na kukosa uelewa.

Aidha Mwanzilishi Mwenza wa Mfuko wa Kupambana na Magonjwa adimu wa Ali Kimara Rare Disease Foundation, Sharifa Mbarak alisema kuwa kupitia tafiti wataweza kubaini vyanzo vya magonjwa hayo na tiba zake.

“ni matumaini yetu kwamba tafiti za kina zinatusaidia kutambua na kubaini tiba sahihi hivyo kupunguza gharama za matibabu,”alisema Mbarak.

Mwanzilishi huyo alitoa mwito kwa serikali na wadau wa maendeleo kusaidia elimu ya nyumbani kwa watoto wenye magonjwa adimu na upatikanaji wa dawa kwa gharama nafuu.

“watoto wenye changamoto za magonjwa haya wanashindwa kuhudhuria masomo ya darasani kama wengine, hivyo kuhitaji kuwa darasa maalum kwa ajili ya kujifunza wakiwa nyumbani ni muhimu sana,”aliongeza mwanzilishi huyo.

Pia aliviomba vyuo vikuu vya tiba kuingiza magonjwa adimu kwenye mitaala yao ili kuwasaidia madaktari vijana kuweza kuyabaini katika hatua za awali.

Kwa upande wake mmoja wa waathirika wa magonjwa adimu, Irene Joel ambaye anaishi na ugonjwa wa Lupus tangu utoto wake aliitaka serikali kuendelea kuwaunga mkono watu wenye matatizo hayo.

Magonjwa adimu, ambayo pia hujulikana kama magonjwa ya watoto yatima, ni kundi la magonjwa ambayo huathiri asilimia ndogo ya watu.

Hali hizi mara nyingi zina sifa ya mchanganyiko wa mambo, ikiwa ni pamoja na kiwango cha chini cha maambukizi na utata wa dalili zao.

Mara nyingi, magonjwa ya nadra ni asili ya maumbile, lakini pia yanaweza kutokana na maambukizi, mambo ya mazingira.