Na Joyce Kasiki,Dar


TAASISI za huduma ndogo za kifedha nchini zimetakiwa kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa mikopo pamoja na kuzingatia misingi ya utawala bora ili kupunguza ongezeko la mikopo chechefu. Udhaifu katika tathmini ya wakopaji na matumizi ya fedha za mikopo kinyume na malengo yaliyokusudiwa umetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia changamoto hiyo.
Wito huo umetolewa na Mfuko wa SELF Microfinance Fund (SELF MF) wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watoa huduma za kifedha, yaliyolenga kuongeza ufanisi wa taasisi hizo katika kusimamia shughuli zake na kuboresha huduma kwa wajasiriamali na wananchi.
Mafunzo hayo yamejikita katika maeneo ya utawala bora, usimamizi wa fedha na taratibu za utoaji na ufuatiliaji wa mikopo.
Akizungumza Novemba 20, 2026, Meneja wa Masoko na Uhamasishaji wa SELF MF, Linda Mshana, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea washiriki uwezo wa kutafsiri taarifa za kifedha, kuelewa misingi ya utawala bora na kusimamia mchakato mzima wa mikopo, kuanzia utoaji hadi urejeshaji. Ameeleza kuwa maarifa hayo yataziwezesha taasisi kutathmini hali yake ya kifedha na kiutendaji, kutambua changamoto mapema na kuchukua hatua za kuzitatua.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Wepan Financial Services Limited, Macdonald Dionizuanga Lwanga, amesema mojawapo ya changamoto kubwa katika biashara ya utoaji mikopo ni baadhi ya wakopaji kutumia fedha walizokopa kwa shughuli tofauti na zile walizoeleza wakati wa kuomba mikopo.
Ametoa mfano wa mfanyabiashara anayekopa kwa ajili ya kuongeza mtaji wa duka lake, lakini baadaye fedha hizo anazitumia kulipia ada za watoto au mahitaji mengine ya kifamilia, hali inayoweza kuathiri maendeleo ya biashara na uwezo wa kurejesha mkopo.
Lwanga ameonya kuwa matumizi yasiyo sahihi ya fedha yanaweza pia kujitokeza ndani ya taasisi za kifedha, pale zinapopata mikopo kwa ajili ya kuendeleza shughuli za utoaji mikopo lakini fedha hizo kuelekezwa kwenye matumizi mengine yasiyokuwa sehemu ya mpango wa awali. Amesema
“Tunashukuru SELF kwa kutuwezesha kupata mkopo ambao unatusaidia kuendesha biashara yetu ya kutoa huduma ndogo za kifedha kwa wafanyabiashara wadogo. Pamoja na kutupatia mkopo, hawajatuacha, wamekuja pia kutujengea uwezo ili tuweze kuwahudumia vizuri wateja wetu.”
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamewapa maarifa kuhusu utawala bora, uandaaji wa hesabu za kifedha na usimamizi wa mikopo katika hatua zake zote.
Naye Meneja wa Tawi la Dar es Salaam la SELF Microfinance Fund, Peter Sambo, amesema taasisi za huduma ndogo za kifedha zina mchango mkubwa katika kupanua wigo wa upatikanaji wa mikopo, hasa kwa wananchi wanaoishi maeneo ambayo mfuko huo hauna matawi. Ameeleza kuwa SELF MF, yenye matawi 12 nchini, imeamua kushirikiana na taasisi hizo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwawezesha kiuchumi kupitia huduma za mikopo.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo unaziwezesha taasisi kupata fedha za kuwakopesha wajasiriamali, kukuza biashara na kuchochea upatikanaji wa ajira.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Izi Trust Microfinance, Philomena Deogratius, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kupata uelewa zaidi kuhusu namna ya kutambua wateja wenye viashiria vya kushindwa kurejesha mikopo kabla ya kuwapatia fedha.
Amesema amejifunza kuwa changamoto za urejeshaji zinaweza kubainika tangu hatua ya awali ya tathmini ya mteja, hivyo ni muhimu kwa taasisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu uwezo wa kifedha na mwenendo wa wakopaji kabla ya kutoa mikopo. Ameeleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza hatari ya mikopo chechefu na kuimarisha uendelevu wa taasisi za huduma ndogo za kifedha nchini.

More Stories
Maajabu ya aliyekatisha masomo kwa ujauzito
Milioni 600 kuwekezwa miundombinu elimu watu wazima
Taasisi zatakiwa kuimarisha utayari dhidi ya El Nino