SERIKALI kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) imeendelea kutoa fursa ya pili kwa wasichana waliokatisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo ujauzito, kurejea katika mfumo wa elimu na kuendeleza ndoto zao za kitaaluma.
Kupitia mpango wa Elimu ya Njia Mbadala, Serikali imeweka mazingira yanayowawezesha wasichana hao kupata elimu kulingana na mazingira yao, hatua inayolenga kuhakikisha changamoto za maisha hazigeuki kuwa kikwazo cha kudumu katika kupata haki ya elimu.
Miongoni mwa wanufaika wa fursa hiyo ni Gladness Lugusi, aliyekatisha masomo akiwa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mlandege mkoani Iringa baada ya kupata ujauzito. Kupitia mpango huo, alipata nafasi ya kurejea darasani katika kituo cha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na kuendelea na masomo licha ya kuwa mjamzito.
Ushirikiano wa walimu ulikuwa sehemu muhimu ya safari yake, kwani alipata msaada wa kitaaluma na kisaikolojia, huku akipatiwa mazingira yaliyomwezesha kuendelea na masomo hata baada ya kujifungua na kuanza majukumu ya malezi ya mtoto.
Matokeo ya juhudi hizo ni Gladness kufanikiwa kuhitimu elimu ya sekondari kwa kupata daraja la tatu na kupata nafasi ya kuendelea na kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Kiwele, mafanikio yanayoonesha umuhimu wa kutoa fursa za elimu kwa vijana wanaokumbana na changamoto za maisha.
Ushuhuda wake unaonesha kuwa uwekezaji wa Serikali kupitia SEQUIP hauishii katika kutoa nafasi ya kurejea shuleni, bali pia unaweka mazingira ya kuwasaidia wanufaika kuendelea na masomo na kufikia hatua nyingine za elimu.
Aidha, ushirikiano kati ya shule, walimu na wazazi unaonesha kuwa kuwawezesha vijana kielimu ni jukumu linalohitaji mshikamano ili kuwapa nafasi ya kujenga maisha yao na kuchangia maendeleo ya jamii.
Safari ya Gladness ni funzo kwa vijana waliokatisha masomo kuwa changamoto za maisha si mwisho wa ndoto zao. Fursa ya pili inapopatikana, ni muhimu kuitumia kwa juhudi, uthubutu na kutokata tamaa ili kufikia malengo waliyojiwekea.

More Stories
Taasisi huduma ndogo za fedha zatakiwa kuimarisha usimamizi mikopo
Milioni 600 kuwekezwa miundombinu elimu watu wazima
Taasisi zatakiwa kuimarisha utayari dhidi ya El Nino