November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balozi wa Italia Nchini Tanzania Mh. Roberto Mengoni(Kulia) na Katibu mtendaji wa Baraza la sanaa la taifa Bw. Godfrey Mngereza(Kushoto) wakifanya uzinduzi wa logo ya swahili Fashion Week kwa msimu huu.

Swahili Fashion Week 2020 yazinduliwa rasmi

Na Angella Mazula, TimesMajira Online

MAONESHO ya mavazi Afrika Mashariki na Kati ‘Swahili Fashion Week & Award 2020’, yamezinduliwa rasmi jana na kumalizika kesho Oktoba 6, katika Hotel ya Serena Jijini Dar es Salaam. Huku likiwa na wabunifu takribani 45 kutoka nchi za Afrika Mashariki na kwingineko ulimwenguni.

Akizungumza na waandishi wa habari, Muhasisi wa ‘Swahili Fashion Week & Awards’, Mustafa Hassanali amesema, Mwaka 2020 umekuwa na changamoto nyingi sana kiuchumi, pamoja na changamoto nyingine zikiwemo janga la Corona.

Hata Hivyo, Hassanali amesema Wabunifu zaidi ya 45, wanatarajia kuonesha ubunifu wao kwenye jukwaa la mwaka huu. Hii ni kwa sababu ya hatua zenye tija na chanya zilizochukuliwa na kiongozi wetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli katika kudhibiti janga la Corona.

“Lengo la kuendeleza tasnia ya ubunifu Afrika bado linabaki mstari wa mbele kwa kupitia jukwaa hili na mtandao wake mkubwa wa vyombo vya habari, watumiaji wa bidhaa za ubunifu wa Tanzania, Afrika na ulimwengu kwa ujumla, sasa wataweza kuona mbadala wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje, na kwa wakati wote tumekua tukitilia mkazo thamani ya bidhaa za ubunifu za Afrika kwa kuhamasisha adhana ya ‘Made in Afrika’ na kutengeneza bidhaa zenye hadhi ya Kimataifa kwa misingi ya Afrika.

“Maonesho haya ya 13 ya ‘Swahili Fashion Week & Awards’, yataendelea kuwa kioo kwa maonesho mengine ya mavazi Afrika kwa wabunifu wa Kitanzania, ukanda wa Afrika Mashariki na hata wale wa Kimataifa kwa mvuto na mandhari yake ya kipekee inayoendana na kauli mbiu ya jukwaa la Tanbua Kinachoipendezesha Afrika Discover What Makes Afrika Beautiful,” amesema Hassanali.

Hassanali ameuhamasisha umma wa Watanzania kupenda kuvaa mavazi yanayobuniwa na wabunifu wa Tanzania (Made in Tanzania ), kwani kwa kufanya hivyo wanakuza vipaji vyao na kuwafanya siku moja kutambulika kama wabunifu wakubwa ulimwenguni.

Kwa upande wake Balozi wa Italia hapa nchini Roberto Mengoni amesema, kwa kipindi cha miaka sita mfululizo wamekuwa wakishirikiana na jukwaa la ‘Swahili Fashion Week & Awards’, kwenye maonesho yao na kwa mara nyingine tena mwaka huu anaungana nao kufanikisha maonesho hayo ya 13.