Na Yusuph Dogossi, TimeMajira Online
BAADA ya kurudi katika ubora wao na kupata ushindi wa goli 4-0 dhidi ya Biashara United, kocha mkuu wa Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), Sven Vandenbroeck amesema kuwakiwango kilichooneshwa na wachezaji wake kinazidi kumpa wakati mgumu wa kuchagua wachezaji wa kuanza hasa katika mechi za nyumbani.
Kocha huyo ametoa kauli hiyo baada ya wachezaji wake ikiwemo waliojiunga na timu hiyo msimu huu waliopata nafasi katika mchezo huo kuonesha kiwango bora kilichowarejesha kwenye makali yao.
Amesema, katika kikosi chake cha wachezaji 29, wote wameonesha kiwango bora katika mazoezi lakini kwa bahati mbaya anaopaswa kuwaanzisha ni 11 tu jambo linalimlazimu kufanya maamuzi magumu.
Mara baada ya mchezo huo dhidi ya Biashara, kocha huyo amebainisha kuwa, atakuwa na wakati mgumu zaidi hasa katika mechi zao za nyumbani ambapo uwanja ni mzuri na ubora waliouonesha ndio hashwa kiwango chao ukilinganisha na mechi za ugenini ambazo viwanja haviwaruhusu kucheza pasi za haraka.
Kabla ya kuanza rasmi kwa msimu huu, kocha huyo alisema kuwa, kikosi chake cha msimu huu ni kizuri zaidi ya kilichopita jambo litakalompa wakati mgumu kuchagua wachezaji wa kuanza katika mechi mbalimbali licha ya kumruhusu kutumia mifumo tofauti.
Kulingana na wachezaji wake hasa washambuliaji, kocha huyo amesema, kazi aliyonayo ni kuamua amtumie yupi katika mechi gani hivyo kila mmoja itabidi akubali kuwa kuna michezo atakosa na anatarajia kila mmoja anatakiwa kutimiza ipasavyo majukumu yake kwani kikosi cha wachezaji zaidi ya 20 ni lazima wengine wakae benchi.
Amesema, jambo kubwa ni mchezaji kutokata tamaa na hiyo ni changamoto kubwa waliyonayo ili kumfanya kila mmoja kujitufa na kuonesha uwezo wa hali ya juu katika kuipambania timu.
Akizungumzia mchezo huo, Sven amesema, kila mtu aliona dhamira ya ushindi waliyokuwa nayo hata katika umiliki wa mchezo huo, lakini pia amefurahishwa na wachezaji wake kutoruhusu goli lolote kwani katika mechi tatu walizocheza mpaka sasa, wameruhusu kuruhusu goli mbili.
“Kabla ya mchezo niliwaambia wachezaji wangu tutachokifanya dhidi ya Biashara ndicho tunachotakiwa kufanya kwenye mechi zote za nyumbani ambapo uwanja ni rafiki, kwasababu mechi za ugenini inakuwa ngumu kucheza hivi kutokana na changamoto za viwanja ambazo hazituruhusu kucheza kama tulivyocheza, ” amesema kocha huyo.
Pia amewapongeza wachezaji wake kutokana na kila mmoja kudhihirisha kuwa ana uwezo wa kufunga na kutoa pasi za mwisho za magoli jambo linalomfanya mwisho wa siku kutotegemea mchezaji mmoja na kumpa uwanja mpana zaidi ya kuchagua kile kinachomridhisha katika mazoezi ikiwemo kutumia mfungani mmoja, wawili, watatu au asitumie kabisa.
More Stories
Naibu Waziri wa Fedha abariki ujio mpya wa Bahati Nasibu
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes