December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sven aanika mkakati kuwamaliza Namungo, Yanga *Kapombe nje wiki nne

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KOCHA mkuu wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) Simba , Sven Vandenbroeck amesema kwa sasa akili yake yote anaelekeza katika mechi zao mbili zijazo dhidi ya Namungo pamoja na ile ya Julai 12 dhidi ya Yanga.

Timu hiyo kesho Jumatano Julai 8 itakuwa na kibarua katika uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa dhidi ya Wenyeji wao Namungo ambao pia utamika kwa ajili ya sherehe za kukabidhiwa Kombe lao la ubingwa wao wa msimu huu ambao pia ni ubingwa wa msimu wa tatu mfululizo.

Baada ya Mchezo huo Simba itatua katika uwanja wa Tiafa Julai 12 kuwakaribishwa Watani wao wa Jadi, Yanga katika mchezo wa Nusu Fainali wa Kombe wa Shirikisho la Azam (Azam Sports Fereration Cup) utakaochezwa saa 11:00 jioni.

Mchezo huo utakuwa ni ‘Derby’ ya tatu ndani ya msimu huu ambapo katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) timu hizo zilitoka sare ya goli 2-2 lakini shughuli ikaja kuwa ngumu kwa Simba baada ya kufungwa goli 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa pili uliochezwa Machi 8.

Ushindi huo uliwafanya mashabiki wa Yanga kuwatambia wenzao wa Simba na kudai kuwa licha ya kuukosa ubingwa wa msimu huu lakini kitendo cha kuwafunga kwao ni ushindi tosha.

Lakini sasa baada ya kukutana tena katika hatua hiyo, mashabiki wa Simba wameweka wazi kuwa, safari hii wapinzani wao wasitegemee mteremko kwani wanachokitaka wao kulipa kisasi kwa Yanga na kutokana na kiwango bora kinachooneshwa na wachezaji wao hivi sasa, basi hakuna kitakachowazuia kwenda fainali kwani wanachokitaka ni kubeba pia na kombe hilo baada ya wachezaji kutimiza kazi zao kwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) kwa masimu wa tatu mfululizo huku wale wa Yanga nao wakisema wamejipanga kuendelea kuwa wababe mbeya ya Simba.

Kocha Sven amesema kuwa, mechi hizo mbili zote ni muhimu kwao hivyo wanapaswa kushinda ili kuudhihirisha umma kuwa bado wana kikosi bora na wanastahili kuwa mabingwa wa nchi kwa mara ya tatu mfululizo.

Amesema, baada ya kumaliza mchezo wao dhidi ya Ndanda, kikosi chao kimeendelea kusalia Mtwara kwa ajili ya maandalizi na kitaondoka kesho asubuhi kuelekea Lindi kwa ajili ya mchezo wao wa jioni dhidi ya wenyeji Namungo.

Baada ya mchezo huo, pia kikosi hicho cha Simba kitarudi tena Mtwara kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao ambapo wataendelea na pgogramu yao ya mazoezi ya asubuhi na jioni.

“Kikosi kitaendelea kubaki hapa Mtwara kujiandaa na mechi yetu ya Jumatano dhidi ya Namungo na ile ya Jumapili ya FA kwani zote ni mechi muhimu kikubwa tunahitaji kucheza vizuri na kuhakikisha tunatoa ushindani mkali kwa wapinzani wetu,” amesema kocha huyo.

Nahodha wa timu hiyo, John Bocco amwweka wazi kuwa, wanaiheshimu Namungo kwakuwa ni moja ya timu zilizoonesha viwango bora msimu huu.

Amesema, kwakuwa wapo katika uwanja wao wanajua kuwa mchezo huo ujtakuwa mgumu na wenye ushindani mkali lakini kwao mchezo huo ni muhimu sana kwakua ni siku watakayokabidhiwa kombe lao hivyo ni muhimu kushinda.

“Tunakutana na timu nzuri tena ipo nyumbani kwaniyo sisi kama wachezaji tupo katika maandalizi yetu ya mwisho na tutahakikisha tunafuata maelekezo ili kuweza kupata ushindi katika siku yetu muhimu ya kukabidhiwa kombe,” amesema Bocco.

Akizungumzia majeraha ya beki wao Shomari Kapombe, Sven amesema kuwa, mchezaji huyo atakuwa nje ya uwanja kwa wiki nne hivyo hatacheza mchezo wowote hadi msimu unamalizika.

Kapombe alipata majeraha hayo baada ya kuchezewa faulo kiungo Frank Domayo katika mchezo wa robo fainali wa FA dhidi ya Azam FC wiki iliyopita ambao ulimalizika kwa Simba kupata ushindi wa goli 2-0.