Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online,Tanga
MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Taifa Zanzibar (SUZA) Profesa Mohamed Makame Haji amesema chuo hicho kimeazimia kuonesha programu mbalimbali kwenye maonesho ya wiki ya elimu,ujuzi na ubunifu yanayofanyika Kitaifa jijini Tanga Kwa lengo la kutekeleza sera na mipango iliyopo kwa Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye maadhimisho hayo, Prof.Makame amesema programu hizo zinakwenda kuangazia hasa kwenye tafiti ambazo zimejiweza zaidi kwenye eneo la utekelezaji wa shughuli zinazoendana na sera ya uchumi wa buluu kama uvuvi, masuala ya gesi asilia na petroli pamoja na mambo mengine.
“Chuo kinaonesha namna gani kinashiriki kikamilifu katika matokeo mbalimbali ya kitafiti na utoaji wa taarifa katika tafiti hizo kwa jamii ili ziweze kutumika kuwa sehemu ya chachu ya kuleta mageuzi na mabadililo ambayo yanapambaniwa kuweza kufikia uchumi ulio bora kwa Taifa, “amesema na kuongeza kuwa
“Tunao hapa wanafunzi wamekuja na bunifu mbalimbali zinaashiria matokeo ya utafiti uliofanyika wa kuandaa suluhisho mbalimbali za kitaalamu kama sehemu ya kutoa suluhisho la changamoto ambazo jamii zetu zinakabiliana nazo, “amesisitiza Prof. Makame.
Pamoja na mambo mengine Prof. Makame amesema vijana wa chuo hicho wana kazi ya kubuni na kuja na suluhisho la aina mbalimbali la kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii, lakini pia kuja na majawabu yanayoweza kutumika kwa jamii na kutoa matokeo makubwa zaidi ya kunufaisha Taifa.
Prof. Makame amesema mbali na hilo, chuo hicho kitaonesha mambo mbalimbali yanayofanywa na taasisi hiyo ambapo sehemu ya masuala hayo ni kukaribisha watafiti na wabunifu, watu mbalimbali, wadau wa elimu waweze kufika kwenye chuo hicho kupata huduma ambazo zinatolewa.
“Moto wa chuo hicho ni kichochea katika mabadiliko ya kijamii na kimejikita hapo kuhakikisha kwamba elimu ya juu inaweza kutumika kikamilifu kuleta mageuzi makubwa yatakayoleta chachu ya maendeleo ya kiuchumi nchini, “
“Katika muda huu ambapo Zanzibar na Tanzania Bara kwa ujumla zimeelekeza nguvu zake katika eneo la sayansi na Teknolojia kwa kutekeleza sera na mipango iliyopo ya kimaendeleo wameazimia katika maonesho hayo kuonesha programu mbalimbali ambazo ndizo hasa zinakwenda kuangalia namna chuo kikuu kilivyojipanga katika utekelezaji wa sera za maendeleo za nchi, “amebainisha Prof.Makame.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba