November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Suma awataka  watoto wenye ulemavu wajione sawa na wengine

Na Esther Macha, Timesmajira,Online,Rungwe

WATOTO wenye ulemavu wanaosoma katika shule maalum ya Katumba Mbili, iliyopo wilayani Rungwe Mkoani Mbeya wametakiwa kujiona sawa na watoto wengine  na kwamba wasijiweke kama vile kwa hali walizonazo, basi hawastahili kabisa jambo ambalo siyo sahihi.

Imeleezwa kuwa watoto hao  wanatakiwa kutiwa moyo ili nao watimize ndoto zao walizonazo katika maisha.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Mbeya , Suma Suma Fyandomo  wakati akizungumza na watoto wanaosoma shuleni hapo, ambapo aliwatembelea na kuwapa zawadi za mchele, maharage, unga wa sembe, sukari, juisi, biskuti ili nao watambue  jamii ipo pamoja nao na haijawatenga.Msaada wote una thamani ya sh.milioni 1.2.

Fyandomo amewataka  watoto hao wasijione kuwa kuzaliwa na ulemavu basi ndiyo dunia imekwisha, hapana kwani watu wenye ulemavu nao wana nafasi kubwa sana kwenye jamii na nchi kwa jumla.

“Niliamua kufika kituoni pale kwa ajili ya kuwatia moyo, ili wasione kuwa ni walemavu basi ndiyo dunia imekwisha, hapana walemavu nao wana nafasi kubwa sana kwenye jamii na nchi kwa jumla” amesema Suma.

Aidha Mbunge huyo amesema kuwa  hata Bungeni wanao wabunge wanaowakilisha watu wenye ulemavu, ambao nao ni walemavu na wapo kwa ajili ya hilo kundi muhimu, na hawa watoto nawatia moyo kuwa wasikate tamaa na huo siyo mwisho wa maisha.

“Niliwatia moyo wasome kwa bidii kwani nao nafasi ya kufanya vizuri wanayo, na wakisoma vizuri hapa watatoka wahandisi, wakurugenzi,wabunge, hata madiwani, kwani kwenye jamii tunathamini kila binadamu hatubagui wala hatuchagui” alisema Fyandomo.

 “Kile kituo hiki ni kikubwa sana kikiwa na watoto wenye ulemavu 230, wakiwemo wenye matatizo ya kusikia (Viziwi), wasioona na uwezo wa kuona (Vipovu), wenye ulemavu wa ngozi (Albino) lakini pia wale wenye ulamavu ambao hawajiwezi kabisa” .

Hata hivyo Fyandomo amesema kwamba  Sadaka siyo lazima uende kutoa kanisani ama msikitini, hivyo niliona ni namna gani na mimi niweze kwenda kuwaona pale nikiwa nimewabebea vyakula na vinywaji.

Akizungumzia kuhusu changamoto za shule hiyo Mbunge Fyandomo alisema  alizoziona kituoni hapo, ni kukosekana kwa maabara, lakini pia hata maktaba hawana huku vitu muhimu vikiwemo vitabu na vifaa vya kufundishia, wasio na uwezo wa kuona ama kusikia, vikiwa vimehifadhiwa kwenye makabati chakavu.