November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sulle ang’ara Hydom Marathon

Na Mary Margwe, TimesMajira Online, Mbulu

MWANARIADHA chipukizi kutoka katika Kata ya Endamilay Wilayani Mbulu mkoani Manyara, Helman Sulle ameibuka mshindi wa mbio za Haydom Marathon kwa upande wa kilometa 21 ‘Half Marathon’ akitumia saa 1:6:13 na kujinyakulia kitita cha Sh. 250,000.

Katika mbio hizo nafasi ya pili ilichukuliwa na Joseph Martin (Babati) aliyekimbia saa 1:6:38 na kuondoka na Sh. 125,000, mshindi wa tatu ni Antony Mwaya (Hanang) aliyekimbia kwa saa 1:6:48 moja na kupata Sh. 75,000, mshindi wa nne ni Ibrahimu Hayuma (Babati) aliyetumia saa 1:8:05 huku mshindi wa tano akiwa Alex Sanga (Mbulu) aliyekimbia saa 1:9:20.

Washindi kwa upande wa wasichana ni Tunu Andrea kutoka Singida aliyekimbia 1:28:16 na kuzawadiwa sh.250,000, Neema Sanka (Babati) aliyekimbia saa 1:32:52 na kupata sh.125,000 mshindi wa tatu ni mshindi wa tatu ni Laura Chuwa (Dkt.Hopitali ya Haydom) alikimbia kwa saa 3:29:45 na kuondoka na Sh.75,000

Kwa upande wa mbio za kilometa 10, mshindi alikuwa Ambross Sadikiel (Mbulu) aliyekimbia dakika 29:50 na kujishindia sh.100,000, mshindi wa pili ni Benson Massawe (Babati) dakika 39:21 na kupata Sh. 50,000, nafasi ya tatu ilichukuliwa na Tobias Bura (Mbulu) aliyetumia dakika 30:54 na kuondoka na Sh.25,000, mshindi wa nne ni Joshua Tsontso (Babati) aliyekimbia kwa Dk 31:16 huku mshindi wa tano akiwa ni Damiano Christin (Arusha) alikimbia kwa dakika 31:39.

Washindi kwa Wasichana Loema Awaki wa Mbulu aliyekimbia dakika 35:54 na kuzawadiwa Sh.100,000, mshindi wa pili ni Paulina Stephano (Hanang) aliyekimbia dakika 40:11 na kupata Sh.50,000, mshindi wa tatu ni Ferista Sulle (Haydom Mbulu) aliyekimbia kwa dakika 40:35 na kuondoka na Sh. 25,000, nafasi ya nne ilikwenda kwa Salome Hiit (Babati) aliyekimbia kwa dakika 40:57 huku nafasi ya tano ikienda kwa Rehema Gwatema (Mbulu) aliyekimbia kwa dakika 47:39.

Akitangaza matokeo hayo mbele ya Askofu wa kanisa LA KKKT Dayosisi ya Mbulu Niclolaus Nsanganzelu, Mkurugenzi Mtendaji wa Tiba wa Hospitali ya Rufaa ya Kilutheri Haydom, Dkt. Paschal Mdoe amesema mashindano hayo yameandaliwa na Hospitali hiyo kwa lengo la kuchangia ujenzi wa wodi ya watoto wachanga.

Mbali na mbio ndefu za Kilometa 21 na kilometa 10 pia kulikuwa na mbio za kilometa 2 ambapo kwa upande wa Wavulana mshindi alikuwa Calvin Akioo (Arusha), mshindi wa pili ni Brayan Musa (Mbulu), mshindi wa tatu ni Ibrahimu Philipo (Mbulu), nafasi ya nne ilichukuliwa na Tumaini Daniel (Mbulu) huku mshindi wa tano akiwa Jackson John (Mbulu).

Kwa wasichana mshindi ni Haika Elihuruma (Haydom Mbulu), mshindi wa pili ni Gradness Eliakimu (Mbulu), mshindi wa tatu ni Neema Damiano (Mbulu), mshindi wa nne ni Urory Paul (Haydom) na nafasi ya tano ilikwenda kwa Jenifa Philip (Haydom) ambao wote walizawadiwa vyeti.

Amesema, kwa mwaka 2020 malengo yao yalikuwa ni kukusanya Sh. milioni 100 ambayo itaunganishwa na milioni 100 iliyokusanya mwaka jana ili waanze ujenze wa jengo jipya la watoto, ambapo hadi jana walifanikiwa kukusanya Sh.40 hivyo wanategemea kukusanya zaidi kwani bado michango inaendelea kukusanywa kutoka kwa wadau.

Ujenzi wa jengo hilo la watoto hadi kukamilika kwake unahitaji jumla ya Sh. milioni 310 na wanatarajia hadi Januari 2021 wawe wameanza rasmi shughuli za ujenzi wa jengo hilo.

“Jengo ambalo lipo na linatumika kwa sasa ni dogo ambalo awali kulikua na watoto kati ya 6-10 kwa siku ambalo lilikua linajitosheleza, lakini mahitaji kwa sasa yameongezeka sana kwa siku sasa hivi tuna watoto kati 20-30 kwa hiyo unakuta kwamba lile jengo halitoshi kabisa, lakini pia namna ya kuwatibu watoto kumeongezeka, teknolojia imeongezeka tunahitaji kufuga vifaa vipya, kwahiyo lile jengo kwakweli kabisa ni kama hatuna jengo, kwahiyo tunataka kujenga jengo jipya kabisa ” amesema Dkt. Mdoe.

Hata hivyo alisema zaidi kabisa wanategemea kupata michango hiyo kutoka ndani ya nchi, nje ya nchi ni kidogo sana, hivyo ameomba wananchi kuweza kujitoa katika uchangiaji wa michago hiyo ili kuweza kufanikiza ujenzi wa jengo hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Mkoani Manyara Hudson Kamoga amesema jitihada nyingi zimefanyika kuhakikisha inapunguza vifo vya watoto wachanga kwa kuwekeza miundombinu lakini kwa kuwekeza taaluma ya wataalam kuhakikisha inapunguza vifo vya watoto wachanga.

Kamoga ambaye alikua mgeni rasmi akimuakilisha mkuu wa wilaya hiyo Chelestino Mofuga ameema bado kumeendelea kuwa na chamgamoto ili kuweza kufikia sifuri ya vifo vya watoto wachanga Kwa juhudi hizo hospitali ya rufaa Haydom ikaona ni vema kuanzisha wodi maalum kwa ajili ya watoto wachanga, kama serikali inawapongeza sana kwa jitihada hizo.

“Niwapongeze sana hospitali ya Haydom kwa kuandaa mashindano haya, kwani tumepata wakimbiaji kutoka sehemu mbalimbali kutoka hapa Haydom, Mbulu yenyewe, Babati, Karatu, Hanang, Arusha, Singida na sehemu zingine, sasa hivi kumekua na mwamko mkubwa sana wa marathon Tanzania, na ukizungumzia mbio Mbulu ni kitovu cha wakimbiaji, wakimbiaji wakubwa walioipa heshima kubwa Tanzania katika medali ya riadha mbulu ni moja wapo kama kina mzee Stivin Akwaari , kina mzee Bariye na wengine wengi wametoka Mbulu wamefahamika na tunataka sasa kurejea katika misingi ya kitovu cha riadha Tanzania na duniani kwa maana ya Mbulu, tutaendeleza hii michezo, tutaendeleza haya mashindano ” amesema Kamoga.

Aidha Kamoga amesema amefurahi kuwa sehemu ya changizo kwa ajili ya ujenzi wa hilo jengo la watoto ambao wanazaliwa huku wakipata changamoto mbalimbali , hivyo aliendelea kutoa wito kwa wananchi nao kujitokeza kuchangia ujenzi huo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Glegory Massay amesema, licha ya kuwa lengo la marathon hiyo ni kuchangia ujenzi huo wa jengo la wodi ya watoto lakini pia Michezo husaidia kuweka miili katika afya bora na kuwa mbali na daktari unauweka mwili katika kiwango stahili.

Massay amesema kuwa, mwili unapokua kwenye mazoezi unaufanya mwili kutoa sumu ambayo mara nyingi huoatikana kwenye ulaji wa vyakula mbali mbali, hivyo michezo hujenga afya, hufanya wqtu wafahamine, michezo pia ni ajira kubwa kwa wenye kuwekeza zaidi katika michezo.