Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
SIKU ya hedhi duniani huadhimishwa kila mwaka, ifikapo Mei 28 . Siku hii ina lengo ya kuwakutanisha wadau mbalimbali kwa dhumuni la kuongeza uelewa kuhusu maswala ya hedhi kwa msichana na kuhamaisha msichana kupata maji safi na taulo hasa wale walio katika mazingira ya hali ya chini.
Sababu wanapoingia katika siku zao za hedhi waweze kujisitiri na kuendelea na taratibu zingine kama kuhudhuria masomo na shughuli nyingine.
Kauli Mbiu ya Siku ya Hedhi mwaka 2022 ‘ Hedhi iwe kama ni moja ya maisha ya kawaida kwa msichana na mwanamke (Making menstruation a normal fact of life by 2030).
Hii ina maana tuwe na dunia ambayo hakuna mtu ataachwa nyuma au atashindwa kufikia malengo yake au kufanya shughuli zake za kila siku kwa sababu tu anaingia kwenye siku za hedhi.
Katika kuadhimisha siku ya hedhi kwa Mkoa wa Mwanza , Shirika la Marie Stopes Tanzania kwa kushirikiana na Flaviana Matata Foundation wametoa elimu ya masuala ya hedhi salama kwa wasichana na wavulana 987 katika shule ya Sekondari ya Bukandwe iliyoko Wilaya ya Magu Mkoa wa Mwaza.
Hata hivyo baada ya mafunzo mashirika hayo yaliwashika mkono wanafunzi hao kwa kutoa zawadi mbalimbali ikiwemo taulo za kike kwa wasichana.
Katika kuadhimisha siku hii wametoa wito kwa mashirika binafsi, Serikali na walimu kusisitiza utolewaji wa elimu ya masuala ya hedhi kwa vijana wa kiume na wa kike kwani elimu hio itamsaidia msichana kutambua mabadiliko ya mwili na kukabiliana nayo pamoja na kufahamu namna ya kujisitiri kipindi anachoingia kwenye hedhi, na kwa mvulana kuelewa mabadiliko hayo kama mshiriki mwenza ili kuondoa unyanyapaa pale msichana anapokuwa kwenye hedhi .
Kwa mashirika ya afya , mashirika ya maendeleo na taasisi mbalimbali kuzisaidia jamii kwa namna mbalimbali kuhakikisha wasichana hasa walio shuleni kunakuwa na mazingira rafiki ili wanapoingia kwenye siku zao za hedhi wasikose mahitaji yao muhimu yatakayowasababisha kushindwa kushiriki kwenye masomo na masuala mengine ya jamii kutokana na hedhi .
‘Kuliangalia suala la utaratibu wa bei za taulo za kike, upatikanaji wa maji safi na salama katika shule , kusaidia maeneo yenye uhitaji ili wasichana waweze kupata taulo za kujisitiri kwa muda wa mwaka mzima ili wasiweze kukosa mahudhurio shuleni,’ alisema Flaviana.
Hedhi salama ni ile ambayo inahusisha mtoto wa kike kupata mahitaji yake yote muhimu akiwa kwenye siku zake za hedhi. Mahitaji hayo huhusisha taulo za kike ama pedi kama ijulikanavyo na wengi, maji safi na salama na sehemu ya kubadilishia.
Naye Meneja Mawasiliano wa Shirika la Marie Stopes Tanzania, Esther Shedafa alisema shirika hilo lenye matawi bara na visiwani, wanasema kuwa mtoto wa kike akipata hedhi salama basi ataweza kuondokana na matatizo mengi ya kiafya kama vile miwasho, fangasi, maumivu pamoja na hedhi bila kutokwa damu nyingi na hivyo huwa hedhi yenye amani na furaha.
Alisema kuwa auala la hedhi halipaswi kuwa kero kwa mtoto wa kike. Hata hivyo, imekuwa tofauti kwa watoto wengi wa kike ambao wamekuwa wakipata wasiwasi na kukosa raha pindi wanapokaribia mzunguko wao. Hii inatokana na changamoto ambazo watoto hawa wa kike wanazopitia katika kupata hedhi salama.
‘Jambo la kusikitisha ni kwamba mara nyingi tumekuwa tukigusia tu masuala ya kiafya pindi tunapozungumzia hedhi salama na kusahau kuwa kukosekana kwa jambo hili kunaweza kuleta athari katika nyanja mbalimbali za maisha ya mwanamke huyu’ alisema Esther.
Aliongeza kuwa baadhi ya mazingira yanayoweza kumkwamisha mtoto wa kike ni pamoja na mila potofu mfano: mwanamke au msichana aliye kwenye hedhi hapaswi kugusa maji, kupika, kushiriki sherehe za kidini au hata za kijami.
Pia fikra hizo potofu husababisha ubaguzi na kuendeleza Imani potofu juu ya wanawake wanapokuwa katika siku zao za hedhi kuwa ni wachafu.
Kutojihusisha katika shughuli mbalimbali za jamii kutokana na kukosekana kwa nyenzo ambazo zitamsaidia mtoto wa kike katika kipindi aonapo hedhi basi mara nyingi watoto hawa hujitenga katika shughuli mbalimbali kama vile shule, michezo, mikutano mbalimbali kwani huona aibu na hofu ya kuonekana kwa watu akiwa na hali ile. Kutojihusisha na shughuli hizi huweza kuleta madhara makubwa sana kwa mtoto huyu wa kike na yanaweza kuwa ya papo kwa papo au ya muda mrefu.
‘Kukosa fursa kama mwanamke atakuwa wa kukaa tu nyumbani kipindi akiwa kwenye siku zake sababu tu amekosa vitu vya kumsaidia kupata hedhi salama basi ni wazi kuwa atakuwa anakosa fursa nyingi sana zinazoweza kujitokeza katika jamii yake kipindi yeye akiwa katika siku zake za hedhi,’ alisema.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu